
MUIGIZAJI Sandra Dacha hatimaye amepata furaha baada ya akaunti yake ya Facebook yenye wafuasi takribani milioni moja kurejeshwa chini ya udhibiti wake.
Kupitia kwa akaunti mbadala, Dacha
alitangaza kupata udhibiti kamili wa akaunti hiyo ambayo imekuwa mikononi mwa
wadukuzi kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Dacha alikumbuka siku ambayo hiyo
akaunti ilipodukuliwa mnamo Februari mwaka jana, alishindwa kulala na hata hamu
yake ya kula ilipotea akabaki akilia bila msaada.
“Februari mwaka jana, ukurasa wangu wa
Facebook ulidukuliwa. Na acheni niwaambie, maisha yangu hayajawahi kuwa sawa
tena. Siku ambayo ilidukuliwa, nilishindwa kula, nilishindwa kulala, nililia,
nikawika na kulia tena,” Sandra Dacha alisema.
Alishukuru usimamizi wa Facebook na
rafiki yake Martin Githinji kwa kuwa wa msaada mkubwa kwake ambapo amekuwa
akifuatilia mchakato wa kurejeshwa kwa akaunti hiyo mikononi mwake.
Alimtania Githinji kwamba kama si hali
ya uchumi wa sasa, angempa zawadi ya Ndege aina ya helikopta.
“Lakini acheni niwaambie, baada ya
panda-shuka zote, ninafuraha kutangaza kwamba akaunti hii imerudi kwangu,
hallelujah. Shukrani zote ziende kwa Martin Githinji na timu ya Facebook.”
“Wewe Marto wewe aki ya Mungu kama sio
huu uchumi ningekununulia chopper. Pole kwa kukusumbua katika muda wote huu,” Dacha aliongeza.
Akaunti hiyo ilidukuliwa ikiwa na
wafuasi 962,000 mnamo Februari 2024 na kumuacha Dacha akiwa anategemea akaunti
ya Kibinafsi kwenye ukurasa huo.