
ALIYEKUWA mpiga picha wa Diamond Platnumz, Lukamba ameibuka kwa mara nyingine, safari hii akielekeza mtutu wake wa mashambulizi kwa bosi wake wa zamani.
Kupitia msururu wa maneno makali kwenye insta stories zake,
Lukamba alidai kwamba wafanyikazi wa Wasafi wote wanalipwa mishahara duni licha
ya kufanya kazi kubwa.
Alisema kwamba miaka 2 tangu aondoke Wasafi, hakuna
mfanyikazi ambaye amevunja rekodi ya kufanya kazi jinsi yeye alikuwa akifanya,
lakini malipo yake ni ya kijungu jiko.
Msanii huyo aliitaja Wasafi kama jehanamu, akimtaka bosi wao
Diamond kuwafanyia haki ya mishahara mizuri watu wanaojimaliza kulitetea jina
lake kama kina Baba Levo.
“Unajitahidi kuaminisha
watu uongo. Kama kuna mtu kavunja rekodi yangu ajitokeze. Nina mwaka wa pili tangu
nitoke jehanamu. Bwana wee hakuna maisha hapo, ni njaa kali sana.”
“Diamond! Diamond nani
wewe, kawa Mungu? Acheni kudanganya watu sasa, nitayamwaga,” Lukamba alitishia.
Alidai kwamba Wasafi ndio huwafanya watu kuwa mstaa lakini akasema
kwamba mwisho wa siku watu hawali na kuishi ustaa na kumtaka Diamond kuboresha
mishahara yao.
“Walipeni watu vizuri,
watu wanajitoa sana wanafanya kazi nzuri ambazo mpaka leo mnajivunia kazi zao. Nani
atakula ustaa bila hela?” Lukamba alihoji.
Alidai kwamba Wasafi imekimbiwa na wafanyikazi wengi kutokana
na uongo, huku pia akidai kwamba baadhi ya wacheza densi ambao waliondoka na
kwenda Marekani wamefanya maendeleo makubwa chini ya mwaka tangu kugura kibarua
cha Diamond.
“Imagine madensa wameng’ang’ana
miaka 10 bila chochote maskini mpaka wamekimbia zao Marekani mwaka mmoja
wameshajenga. Wangekufa njaa,” aliongeza.
Lukamba pia alikariri kwamba ufichuzi huo wake si wa kutafuta
kiki akisema kwamba watu wa Wasafi kina Baba Levo ndio walioanza kumshambulia.