
SIKU chache zilizopita, video ya mchungaji David Ibiyeomie wa Salvation Ministries nchini Nigeria akihubiri kwamba Yesu hapendi watu maskini na hakuwahi tembelea mtu maskini na kuingia katika nyumba yake ilizua mjadala pevu mitandaoni.
Watu mbali mbali wameichambua video hiyo na kutoa majibu yao,
baadhi wakihisi kwamba mchungaji huyo alikuwa anawapotosha waumini wake kuhusu
chuki ya Yesu kwa maskini.
Mmoja kati ya wakosoaji wa mahubiri hayo ni kasisi wa kanisa
katoliki kutoka nchini Nigeria, Chinaka Justin Mbaeri ambaye anahisi pasta
David Ibiyeomie alivuka mipaka katika kile anahisi ni kudanganya kondoo wa
Bwana.
Kasisi huyo wa Katoliki alitumia mifano kutoka vifungu
mbalimbali vya Biblia kumpiga misururu wa makumbo pasta huyo akimkosoa kuhusu
kueneza dhana ya Yesu kuchukia maskini.
“Madai ya kwamba “Yesu
hakuwahi kumtembelea maskini yeyote katika nyumba yao” na kwa hiyo “Anachukia
umaskini” si ya uwongo tu bali ni ya kupotosha kwa hatari.”
“Inapotosha maisha ya
Kristo na huduma yake thabiti kwa maskini. Utume wa Yesu, kama ulivyofunuliwa
katika Maandiko na kuthibitishwa na Kanisa, ulielekezwa haswa kwa maskini,
waliotengwa, na wa hali ya chini (rej. Luka 4:18) - "Roho wa Bwana yu juu
yangu ... amenitia mafuta kuwahubiri maskini Habari Njema." Hakuwavumilia
tu maskini, aliwatanguliza - chaguo la upendeleo kwa maskini (rej. Mathayo
11:5)” kasisi alieleza.
Alinukuu kifungo kingine cha kueleza kwamba Yesu alizaliwa
katika familia ya umaskini na hivyo haileti maana kuzua dhana kwamba hapendi
watu maskini wakati wazazi wake walikuwa watu wa maisha ya kawaida tu.
“Yesu alizaliwa katika
umaskini, amevikwa nguo za kitoto, na kulazwa horini (Luka 2:7). Alikula pamoja
na watoza ushuru na wenye dhambi, naam, lakini pia na wakulima wanyenyekevu,
wavuvi, na watu waliotengwa. Hakuchagua mali wala maisha ya ikulu. Je, tuseme
Alijichukia Mwenyewe?” Kasisi Mbaeri alihoji.
Kasisi huyo alikosoa Kauli ya pasta kwamba Lazaro hawakuwa
maskini na ndio maana Yesu alipowatembelea nyumbani kwao walimpa chakula,
akisisitiza kwamba Biblia yenyewe inawatambulisha kama maskini.
“Kudai kwamba Yesu
alimtembelea Lazaro wa Bethania, ndugu ya Mariamu na Martha, na kwamba walikuwa
wakimpa chakula, haimaanishi kwamba walikuwa matajiri. Hii inafichua upuuzi wa
Mchungaji Ibiyeomie wa maana ya mji wa nyumbani wa Lazaro, ambao ni Bethania.
Bethania kwa Kiebrania ni "Beth anya" (בֵּית עַנְיָה), ambayo ina
maana ya "Nyumba ya Maskini" au "Nyumba ya Mateso."
Katika video hiyo ya kama dakika moja hivi, mchungaji David
Ibiyeomie alidai kwa ukakamavu kwamba Yesu hapendi maskini ndio maana
hakuwatembelea katika miaka yake 33 ya huduma duniani.
"Yesu hakuwahi
kumtembelea maskini yeyote katika Biblia. Chunguza Biblia yako. Yesu hakuwahi
kuingia katika nyumba ya mtu maskini. Hiyo ina maana anachukia umaskini.
Angalia, alimtembelea Lazaro, hawakuwa maskini walikuwa wakimpa chakula.
Alimtembelea Mwenye dhambi aitwaye Zakayo, ambaye alikuwa tajiri. Niambie
maskini mmoja Yesu aliingia nyumbani kwake? Anachukia umaskini, hiyo ndiyo
maana - Anachukia watu ambao sio maskini…”
Kama ulikosa video hiyo, itazame kwenye chapisho letu la
awali hapa: