
NAIROBI, KENYA, Septemba 5, 2025 — Muumba maudhui Mitchelle Joyce Akoth Oruko, anayejulikana kama Mjaka Mfine, amesimulia jinsi alivyoapokonywa wig yake ya thamani ya Ksh17,000 na wahalifu waliomvamia katikati ya jiji la Nairobi mnamo Jumatano, Septemba 3, 2025.
Kisa cha Mjaka Mfine kimezua mjadala kuhusu usalama wa wakazi wa Nairobi, huku serikali ikiahidi msako mkali dhidi ya magenge ya uhalifu yanayotisha wakazi.

Mjaka Aporwa Katikati ya Jiji
Akizungumza na Milele FM, Mjaka alisema alikuwa akipita eneo la Moi Avenue alipovamiwa ghafla na watu waliompora wig yake. Alifichua kuwa wig hiyo ya nywele asilia alinunua kwa Ksh17,000.
“Human hair inaanza na Ksh15K and above. Yangu ilikuwa Ksh17K,” alisema kwa uchungu.
Kisa hicho kimeamsha hisia kali mitandaoni, wengi wakieleza mshangao wao kuhusu ujasiri wa magenge yanayowavamia watu mchana kweupe.
Wimbi la Uhalifu Nairobi CBD
Ripoti zinaonyesha magenge yanaendesha visa vya uporaji mchana hadharani, hususan barabarani kama Moi Avenue, Kimathi Street na karibu na migahawa maarufu.
Baadhi ya wahalifu hujitokeza kama watoto wa mitaani au wapita njia wa kawaida, kisha ghafla kuvamia na kuwapora watu.
Kuna wanaotishia kuwapaka kinyesi waathiriwa wakikataa, huku wengine wakitumia dawa za kuwapoteza fahamu kabla ya kuwapora.
Video zinazosambaa mtandaoni zinaonyesha wakazi wakizungukwa na kuporwa mbele ya umati bila msaada wowote, ishara ya jinsi magenge haya yamepata ujasiri na kujiamini.
Serikali Yaahidi Msako Mkali
Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, ametangaza msako mkali dhidi ya makundi ya wahalifu.
Ameelekeza maafisa wa usalama kuongeza doria na kuwafuatilia wahalifu wanaoendesha mashambulizi.
“Serikali haitavumilia ulegevu katika ulinzi. Tayari baadhi ya washukiwa wamekamatwa, na tunawaonya wanaojificha kama watoto wa mitaani kwamba hawatapewa nafasi,” alisema Murkomen.
Aidha, aliongeza kuwa magenge haya yanatumia mbinu za kisiri na kujificha, jambo linalofanya mapambano dhidi yao kuwa changamoto kubwa.
Wakazi Wazidi Kuishi kwa Hofu
Hofu imezidi kutanda kwa wakazi wa Nairobi, wengi wakikiri sasa wanaepuka CBD baada ya giza na hata mchana wanatembea wakiwa macho zaidi.
“Ukienda town lazima uangalie nyuma kila dakika. Hawa watu wamekuwa wengi na hawana hofu ya polisi,” alisema mmoja wa wakazi aliyezungumza na gazeti letu.
Baadhi ya wananchi wameitaka serikali kuimarisha kamera za ulinzi na kuhakikisha askari wanapatikana kila barabara kuu, ili kupunguza visa vya uporaji.
Changamoto za Kukabiliana na Magenge
Wataalamu wa usalama wanasema magenge haya yamepata ujasiri kutokana na mapengo katika utekelezaji wa sheria na ongezeko la ukosefu wa ajira mijini.
Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni, zaidi ya asilimia 60 ya visa vya uporaji mjini hutokea kati ya saa nne asubuhi na saa moja jioni – muda ambapo barabara huwa na msongamano mkubwa wa watu.
Sauti za Mitandaoni
Baada ya kisa cha Mjaka, mitandao ya kijamii ilijaa mijadala na kejeli. Wengine walimwonea huruma, huku baadhi wakishangaa vipi wig ya Ksh17,000 ikawa kivutio kikuu cha wezi.
“Mjaka ametufungua macho. Kama wig inaweza kuporwa mchana, basi simu na pochi ziko hatarini zaidi,” aliandika mtumiaji mmoja wa X (zamani Twitter).