Jumatatu, wanandoa mashuhuri Kelvin Kioko almaarufu Bahati na Diana Marua walichapisha video ya mazungumzo ya wazi waliyoshiriki.
Katika video hiyo, walizungumzia masuala mbalimbali yanayohusu maisha yao na hata kufichua baadhi ya siri kuhusu maisha yao ya nyuma.
Wawili hao pia walishiriki majadiliano kuhusu nani anapaswa kufanyiwa utaratibu wa kupanga uzazi kwa vile wamemaliza kupata watoto huku Bahati akimshinikiza mama huyo wa watoto wake watatu kufunga tumbo lake la uzazi.
"Mimi sitaki kupata mtoto mwingine. Saa hii tayari tuko na timu ya raga," Bahati alilalamika.
Mwimbaji huyo wa nyimbo za kimapenzi aliendelea kumwambia mkewe, "Je, unanipenda? Kwa sasa, kipimo halisi cha mapenzi ni ikiwa tumbo hili la uzazi ni langu, basi ulifunge."
Diana Marua hata hivyo alionekana kupinga sana kile ambacho baba huyo wa watoto wake watatu alikuwa akidai kutoka kwake.
Bahati alisema tamanio lake ni mkewe kutokuwa na uhusiano wa kimapenzi wala kumzalia mwanamume mwingine wakati akifa.
"Nikifa leo, nataka uende hospitali ufanyiwe upasuaji ufungwe. Kila kitu kilicho changu ufunge. Wewe uwe unaishi tu hii dunia bila chochote," alisema.
Mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili alitangaza kwamba ikitokea Diana Marua ashiriki uhusiano wa kimapenzi na mwanamume mwingine baada ya kifo chake basi atarudi duniani kama mzimu na kumsumbua.
Diana hata hivyo alimwomba mwimbaji huyo afanyiwe upasuaji wa kupanga uzazi (Vasektomi) mwenyewe kwani pia yeye hangetaka apate watoto na wanawake wengine. Bahati hata hivyo alieleza wasiwasi wake kuhusu kufanyiwa utaratibu huo.
"Jambo pekee linalofanya niogope kufanyiwa vasektomi ni kwamba naweza fanyiwe alafu hata uume ukatae kusimama," Bahati alisema.
Diana Marua alimkumbusha mwanamuziki huyo kuwa awali aliweka wazi kwamba anatazamia kupata watoto 10 na kumbainishia kuwa uamuzi wa kufunga uzazi huenda ukaathiri tamanio hilo katika siku za usoni.
"Kwa sasa tumbo langu limekupatia watoto watatu pekee. Kwa hivyo unataka nifunge tumbo langu alafu baadaye ukuje kusema tulifanya uamuzi mbaya eti nikuruhusu uende nje na nitafute watoto wengine saba," alilalamika.
Mwishowe, mama huyo wa watoto watatu aliweka wazi kuwa hayuko tayari kufungwa kwa tumbo lake la uzazi kwa ajili ya Bahati akibainisha kwamba tayari amemfanyia vya kutosha kuboresha maisha yake.