Jaji mkuu Martha Koome amekosoa mchakato wa marekebisho ya katiba maarufu BBI akisema kwamba kanuni za kisheria zilikiukwa.
Koome amekuwa wa kwanza kati ya majaji saba ambao wanatarajiwa kutoa uamuzi wao kuhusu sheria ya mfumo wa kimsingi [basic structure]katika mchakato wa kubadilisha vipengele vya katiba.
"Sheria ya mfumo wa kimsingi haiwezi kutumika hapa Kenya, kwa hiyo mabadiliko yoyote yanapaswa kufanywa tu kulingana na katiba," Koome alisema.
Alizilaumu mahakama kuu na ile ya rufaa kwa kutochunguza na kubaini upungufu wa sheria hiyo ya 'basic structure' na kupuuza hali halisi kwamba katiba ya Kenya inaweza kujisimamia.
Alisisitiza kuwa kumekuwa na hatua kadhaa za kujaribu kuifanyia katiba ya 2010 marekebisho bila mafanikio, hali ambayo inadhihirisha uthabiti wake.
Kulingana na Koome, alitaka kuwepo kwa uwezekano na usawa katika kubadilisha au kutobadilisha vipengele katika katiba.
Hata hivyo, alikubaliana na mahakama hizi za upeo wa chini kwamba rais Uhuru Kenyatta hawezi kuasisi mchakato wa kufanya marekebisho kwenye katiba.
Aidha, alisema kwamba Rais Kenyatta kama Mkenya ana kila haki ya kusimamia na kuasisi mchakato wa kubadilisha vipengele kwenye katiba.