logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Zuchu adai kushindanishwa na Lady Jaydee kimziki ni kukosa heshima

Mpaka sasa, Zuchu anasalia kuwa msanii wa pekee wa kike kusainiwa katika lebo ya Wasafi inayoongozwa na Diamond Platnumz - anayedaiwa kuwa mpenzi wake pia.

image
na MOSES SAGWEjournalist

Dakia-udaku29 October 2024 - 10:48

Muhtasari


  • ‘Kunishindanisha na mimi na dada zangu waliotengeneza njia kama dada Komando (Lady Jaydee) ni kuivunjia heshima tasnia. Nakomesha mijadala hii mara moja,” aliongeza.
  • Kwa wakati Fulani, uvuni ulizuka kwamba kulikuwepo na bifu kati yake na Nandy, suala ambalo wote walijitokeza kimasomaso kulikanusha vikali.

Msanii malkia wa Bongo Fleva kutoka lebo ya WCB Wasafi, Zuhura Othman Soud maarufu kama Zuchu amepiga chini mijadala yoyote inayolenga kumshindanisha na mkongwe Lady Jaydee.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Zuchu alionekana kutupa dongo kwa jamaa mmoja aliyelenga kuibua mjadala akitaka kujua kwa nini anahisi Zuchu ni mtunzi mzuri wa mashairi ya Bongo Fleva kumliko gwiji, Lady Jaydee.

Akimfokea kwa ukali wa simba, Zuchu alisema kwamba hata kidogo hawezi kutoa kibali cha kushindanishwa na kina dada wenzake, haswa wale waliotangulia katika kutengeneza njia kwa wanawake wengine katika Sanaa ya muziki wa Tanzania, ambao kwa idadi kubwa umetawaliwa na wasanii wa kiume.

Zuchu alisema kuwa Lady Jaydee ni moja kati ya wasanii waliowaaminisha wasichana wengine wadogo kwamba wanaweza kutoboa katika tasnia hiyo, hivyo kujaribu kumlinganisha naye si tu kumkosea heshima mkongwe huyo bali pia ni kuikosea heshima tasnia nzima ya Bongo Fleva upande wa wasanii wa kike.

“Huu ni mjadala usio na mashiko na wa kijinga kuwahi kutokea. Lady Jaydee ni moja kati ya role models wangu, nampa heshima kubwa sana sababu yeye ni moja kati ya mfano bora sana tuliyo nayo kwenye tasnia especially mabinti,” Zuchu alicharuka.

‘Kunishindanisha na mimi na dada zangu waliotengeneza njia kama dada Komando (Lady Jaydee) ni kuivunjia heshima tasnia. Nakomesha mijadala hii mara moja,” aliongeza.

Tangu ujio wake kwenye tasnia ya muziki wa Bongo Fleva, mrembo huyo amekuwa akilinganishwa na kushindanishwa mara kwa mara na wasanii wengine wa kike, wakiwemo aliowakuta kwenye tasnia na waliokuja nyuma yake.

Kwa wakati Fulani, uvuni ulizuka kwamba kulikuwepo na bifu kati yake na Nandy, suala ambalo wote walijitokeza kimasomaso kulikanusha vikali na hata kuonyesha ukaribu wao si tu kupitia mitandao ya kijamii bali pia katika matamasha mbalimbali yaliyowahusisha wasanii wa kike chini ya mwavuli wa rais Samia Suluhu Hassan.

Mpaka sasa, Zuchu anasalia kuwa msanii wa pekee wa kike kusainiwa katika lebo ya Wasafi inayoongozwa na Diamond Platnumz - anayedaiwa kuwa mpenzi wake pia.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved