Siku ya Ijumaa, Novemba 22, malkia wa bongofleva Zuhura Othman Soud almaarufu Zuchu alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 31.
Watu wengi wakiwemo marafiki, familia na mashabiki walimsherehekea msanii huyo wa WCB alipokuwa akiadhimisha siku yake maalum.
Hata hivyo, bosi wake na mpenzi wake wa siku nyingi Diamond Platnumz alionekana kupuuza siku hiyo maalum, tofauti na siku za nyuma.
Hakukuwa na kitu maalum kilichoonekana kutoka kwa Diamond kwa Zuchu, iwe ujumbe mzuri, zawadi au sherehe. Hii haikuwa ya kawaida kwani wawili hao wanafahamika kuwa na uhusiano wa karibu sana na wamekuwa wakisherehekea kwa nyakati tofauti.
Haya yanajiri wiki chache tu baada ya binti huyo wa Khadija Kopa kutangaza kuachana na bosi wake.
Mapema mwezi huu, Zuchu alitangaza mwisho wa mahusiano yake wa miaka mitatu na bosi wake Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz.
Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Instagram, binti huyo wa malkia wa Taarab, Khadija Kopa alisema kuwa uamuzi wa kutengana ulikuwa ni makubaliano ya pande zote mbili.
Aliongeza, "Huu ulikuwa uamuzi wa pande zote mbili, tuna mradi ujao kwa hivyo usishangae utakapotolewa."
Zaidi ya hayo, mwimbaji huyo mrembo mwenye sauti ya kusisimua alimtakia kila la heri Diamond ambaye pia ni bosi wake wa WCB katika shughuli zake zijazo.
Aidha, alidokeza kuwa sasa atazingatia uponyaji na kazi yake.
"Ninawaomba watu wangu wema kuwa na sapoti yenu isioisha kwani lengo langu kuu sasa ni uponyaji na kazi yangu. Wako mwaminifu, Zuchu," alisema.
Mastaa hao wawili wa bongofleva wamekuwa wakichumbiana waziwazi na kuonyesha mapenzi yao kwa takribani miaka mitatu iliyopita. Wamesafiri pamoja, wakapeana zawadi za bei ghali, wakabusiana hadharani, na kuoneshana mapenzi mengine.