Eric Omondi azindua afisi ya Muungano wa Wahitimu na Wajasiriamali Wasio na Ajira nchini Kenya

" Watu wako na vyeti lakini hawaka ajira kwa sababu pengine hawajui au hawana mtu wa kuwashika mkono. Ninaamini kama tutawaunganisha waajiri kwa waajiriwa, tutakwua tumesaidia familia nyingi ,” Omondi alisema.

Muhtasari

• Ofisi hizo zilikuwa na nembo ya mkono wa mhitimu pamoja na rangi ya samawati, Omondi akisema kuwa ni kutokana na vuguvugu la Sisi Kwa Sisi.

Eric Omondi
Eric Omondi
Image: Instagram

Wiki chache baada ya kufanya mkutano mkubwa na wahitimu wasio na ajira nchini Kenya, mchekeshaji aliyegeukia uanaharakati Eric Omondi amefungua ofisi kwa ajili ya kuwashughulikia wahitimu hao kupata ajira.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Omondi aliweka video akiwa mbele ya majengo ya ofisi hizo ambazo alizizindua mapema asubuhi ya Jumatatu.

Alisema kwamba ofisi hizo zitatumika kama sehemu ya mtu yeyote mwenye ajira ambaye anawatafuta wafanyikazi kupeleka maombi yake na kuorodhesha vigezo anavyovitaka kwa mfanyikazi anayemtafuta.

Kisha ofisi hiyo ingechambua mamia ya vyeti vya wahitimu wasio na ajira ambavyo viyakuwa vinapelekwa kule vile vile na wahitimu wanaotafuta kazi, kisha kuwaunganisha na waajiri wao watarajiwa.

Ofisi hizo zilikuwa na nembo ya mkono wa mhitimu pamoja na rangi ya samawati, Omondi akisema kuwa ni kutokana na vuguvugu la Sisi Kwa Sisi.

“Wiki chache zilizopita, nilikutana na idadi kubwa ya wahitimu wasio na kazi, na walikuwa takribani elfu 5. Na niliwaahidi kazi, na leo niko hapa kuzindua muungano wa wahitimu na wajasiriamali wasio na kazi nchini Kenya.”

“Na leo ninatoa ombi kwa Wakenya wenye moyo wa kusaidia, nawaomba kuwasaidia ndugu na dada zetu, sisi ndio walinzi wa ndugu zetu. Watu wako na vyeti lakini hawaka ajira kwa sababu pengine hawajui au hawana mtu wa kuwashika mkono. Na mimi ninaamini kama tutawaunganisha waajiri kwa waajiriwa, tutakwua tumesaidia familia nyingi na kufanikisha watoto kwenda shuleni na pia kuweka chakula mezani mwao,” Omondi alisema.

Alionyesha majengo hayo hadi ndani kwenye sehemu ya mapokezi ambapo alisema wenye ajira watakuwa wanapeleka maombi yao ya kutafutiwa wafanyikazi.

Wiki mbili zilizopita, Omondi alitangaza kufanyika kwa mkutano katika mgahawa mmoja Thika Road kuwajumuisha wahitimu wote wasio na ajira.

Baada ya mkutano huo, Omondi alisema kwamba alishangazwa kuona idadi kubwa ya vijana wenye vyeti vingi mikononi pasi na senti mifukoni mwao.

Alisema kwamba aliwaahidi kuwatafutia kazi kadri ya uwezo wake, na wiki mbili baadae, amezindua ofisi ya KAUGE kuwasaidia kuwaunganisha na waajiri watarajiwa.