Familia ya aliyekuwa mkurugenzi wa wa ICT wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC), Chris Msando imeadhimisha miaka sita tangu kuawa kwake.
Familia hiyo, mnamo Julai 28, 2023 kwa ujumbe wa rambirambi katika gazeti la Nation, iliweka kumbukumbu ya miaka sita tangu Msando alipopatikana ameuawa siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 2017.
Ni miaka sita sasa tangu mwili wa Chris Msando, aliyekuwa akisimamia mifumo ya dijitali ya kupeperusha matokeo ya uchaguzi katika Tume ya IEBC ulipopatikana ukiwa na alama za kuteswa kabla ya kuuliwa.
“Tunapoadhimisha mwaka wa sita wa kuondoka kwako, tunakumbuka kwa furaha nyakati tulizoshiriki pamoja. Uwepo wako unaweza usiwe nasi tena, lakini upendo wako na kumbukumbu zako nzuri ulizoziacha zinaendelea kuangaza mioyoni mwetu,” sehemu ya ujumbe wa rambirambi ilisoma.
Familia hiyo iliongeza kwamba Bw Msando aendelea kupumzika kwa amani na kwamba upendo wao kwake bado uliongezeka kukua.
Kulingana na uchunguzi wa maiti, Bw Msando anadaiwa kuteswa na kunyongwa hadi kufa.
Mwanapatholojia Mkuu wa serikali alisema kuwa afisa huyo wa zamani wa IEBC alikuwa na mikwaruzo mgongoni na mikononi. Alikuwa msimamizi wa mfumo wa upigaji kura wa kompyuta katika uchaguzi wa 2017.
Mwili wake uligunduliwa karibu na maiti ya mwanamke aliyejulikana kama Bi Carol Ngumbu katika msitu viungani mwa mjini wa Nairobi.
Katika mahojiano yake ya mwisho kwenye kituo kimoja cha runinga nchini, Bw. Msando alikuwa amesema kwamba walikuwa wamejiandaa vya kutosha kwa uchaguzi mkuu wa 2017.
"Hakuna udanganyifu, hakuna udukuzi na hakuna udanganyifu wa kura wakati huu," Msando alihakikishia. "Kila kitu kimewekwa kwa njia ambayo mtu mmoja tu ana nenosiri ambalo linadhibiti utiririshaji wote wa matokeo."
Wafula Chebukati, aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC, alisema ilikuwa wazi kuwa Msando aliteswa kabla ya kuuawa.
