Familia hiyo pia ina wanasiasa lakini sio wenye jazba ya kuvutia kama Marehemu baba yao. Moi alimuoa Lena Moi, binti ya mkulima mmoja mashUhuri na mhubiri huko Eldama Ravine Paul Bomet mwaka wa 1950. Pamoja walipata watoto wanane –wavulana watano na wasichana watatu. Lena alikuwa mwalimu lakini baadaye akaamua kusalia nyumbani kuwatunza wanawake na pia kumsaidia Moi aweze kuzingatia taaluma yake katika siasa .
Mtoto wa Moi anayejulikana sana ni kitinda mimba seneta wa Baringo Gideon Moi aliyezaliwa mwaka wa 1964. Gideon alionekana kupendwa sana na Mzee Moi na amechukua jukumu la kuwa msemaji wa Familia kubwa ya Moi. Kifungua mimba wa Moi ni msichana Jenniffer Chemutai Kositany aliyezaliwa mwaka wa 1953 na alisomea katika shule ya Kenya High kabla ya kuelekea marekani kwa masomo ya chuo kikuu. Amesalia kuendeleza maisha ya kibinafsi bila kuangaziwa sana. Jennifer ni mjane na aliolewa na Stephen Kositany ambaye alitokea familia maarufu kisiasa huko Nandi na aliaga dunia katika ajali ya barabarani .
Marehemu Stephen ni kakake mbunge wa sasa wa Soy Caleb Kositany . Jonathan Moi aliyekuwa akipenda sana kuendesha magari ya mashindano ndiye mtoto wa pili na mvulana mkubwa wa Mzee Moi na aliaga dunia aprili mwaka wa 2019 baada ya kuugua saratani kwa muda mrefu .inaripotiwa alikuwa karibu sana na mamake ,Lena kuliko alivyokuwa na mzee Moi .John Mark, mwanawe wa tatu wa mzee Moi ndiye ambaye hafahamiki sana na wengi .Alizaliwa mwaka wa 1958 na kaishi marekani kwa muda akisoma lakini akarejea nchini kabla ya kutamatisha masomo yake. Wanawe wengine wa Moi ni mbunge wa sasa wa Rongai Raymond Moi na mapacha Philip na Doris waliozaliwa mwaka wa 1962.
Philip ni meja mstaafu wa jeshi na alikuwa miongoni mwa wakenya wachache walioanzisha mchezo wa mbio za farasi. Amepata kibarua kigumu kortini katika kesi yake ya talaka ambapo mke wanayetengana naye Rosana Pluda alitaka kulipwa shilingi milioni 90 za matumizi kila mwezi .
Doris, kwa upande wake amedumisha maisha ya faraghani lakini anahudumu katika bodi kadhaa za shule zinazohusishwa na mzee Moi . Alisomea shule ya msingi ya Nairobi, Limuru Girls na baadaye Imani School Thika kabla ya kwenda kuishi Australia kwa muda. Doris pia ni mjane na aliolewa na rafikiye kakake Jonathan katika mbio za magari Simon Choge .
Choge aliaga dunia katika ajali ya barabarani .June, bintiye mdogo Moi ni mtoto wa kulelewa. Kama Gideon alikuwa amependwa sana na Mzee Moi . Alisomea Nairobi Primary, Kenya High School kisha akaelekea chuo kikuu Canada. Ni mfanyibiashara mashuhuri.
Mzee Moi na Mama Lena walitengana mwaka wa 1974 na kisha kutalakiana mwaka wa 1979. Rais mstaafu hakuoa tena . Lena aliishi Rongai kwa maisha tulivu alikofariki mwaka wa 2004. Licha ya kila mmoja kuishi kivyake kwa miaka 30, alizikwa katika shamba kubwa la Moi la Kabarak .





© Radio Jambo 2024. All rights reserved