logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Rais Kenyatta apeleka ujumbe wa maendeleo kwa wakaazi wa Mombasa huku akizindua miradi mitatu

Hafla ya pili katika ratiba ya Rais ilikuwa kuzinduliwa kwa ujenzi wa Daraja la Makupa katika Kaunti ya Mombasa kwa gharama ya shilingi Bilioni 4.5.

image
na Radio Jambo

Habari10 December 2020 - 16:41

Muhtasari


  • Rais alisisitiza kwamba njia ya pekee ya kubuni ajira na kuimarisha uchumi wa nchi ni kukuza sera ya “Nunua Kenya, Jenga Kenya.”
  • Hafla ya pili katika ratiba ya Rais ilikuwa kuzinduliwa kwa ujenzi wa Daraja la Makupa katika Kaunti ya Mombasa kwa gharama ya shilingi Bilioni 4.5.

 Na PSCU

Rais Uhuru Kenyatta leo alipeleka ujumbe wa maendeleo kwa wakaazi wa Kaunti ya Mombasa huku akizindua miradi mitatu katika kaunti hiyo.

Mradi wa kwanza katika ratiba ya Rais iliyojawa na shughuli ni kuzinduliwa kwa kuundwa kwa gari dogo humu nchini aina ya Proton Saga kutoka Malaysia katika mtambo wa Associated Vehicle Assemblers (AVA) huko Miritini Kaunti ya Mombasa.

 

Akihutubia wafanyikazi wa AVA, Rais Kenyatta alipongeza kampuni ya Simba Corporation, yenye idhini ya kutengeneza magari ya Proton hapa nchini na pia kampuni zingine zote za kuunda magari kwa kuunga mkono ajenda ya serikali ya kufufua viwanda vya kutengeneza magari ili kusaidia uchumi na kubuni nafasi za ajira kwa vijana wa Kenya.

“Furaha yangu ni kwamba tunazindua ufufuzi wa utengenezaji wa gari dogo katika kiwanda chenu baada ya kukwama kwa miaka 25. Kufuati hatua hii, tunasherehekea kurejea kwa utengenezaji wa magari madogo hapa AVA Jijini Mombasa na nataka kuwapongeza wote mliohusika,” kasema Rais.

Rais Kenyatta, ambaye aliandamana na Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho, alikariri kujitolea kwa serikali kufufua sekta ya utengenezaji magari hapa nchini kama njia moja ya kuafikia nguzo ya utengenezaji bidhaa katika Nguzo Nne za Ajenda Kuu ya Maendeleo nchini kufikia mwaka wa 2030.

“Tunataka kufufua viwanda vya kutengeneza magari nchini. Kwa wakati mmoja kiasi kikubwa cha magari yaliyokuwa kwenye barabara zetu hakika yalitengenezwa na wakenya chipukizi,” kasema Rais.

Alisikitika kwamba ulafi na kukosa maono kulisababisha soko la Kenya kutawaliwa na magari makuukuu, hali ambayo ilisababisha kufungwa kwa kampuni za humu nchini na kupotea kwa ajira.

“Leo, tunasema tunataka kazi hizo zirudi Kenya. Tunataka vijana wetu kuajiriwa kupitia utengenezaji wa bidhaa humu nchini,” kasema Rais.

Rais alisisitiza kwamba njia ya pekee ya kubuni ajira na kuimarisha uchumi wa nchi ni kukuza sera ya “Nunua Kenya, Jenga Kenya.”

 

Hafla ya pili katika ratiba ya Rais ilikuwa kuzinduliwa kwa ujenzi wa Daraja la Makupa katika Kaunti ya Mombasa kwa gharama ya shilingi Bilioni 4.5.

Itakapokamilika mwezi Januari mwaka wa 2022, daraja hili lenye safu nne linayopita juu ya bahari litachukua nafasi ya daraja la Makupa Causeway lililojengwa mwaka wa 1929. Hatua hii itatoa nafasi ya kubomolewa kwa daraja la Makupa Causeway na kurejesha maisha ya wanyama na mimea katika sehemu hiyo ikiwemo kutiririka kwa urahisi kwa maji ya bahari na kurejesha maisha ya viumbe wa baharini.

Akihutubia wakaazi wa eneo hilo na wafanyikazi wa mradi huo Rais alihakikisha kwamba serikali itaendelea kuzindua miradi ya mabadiliko kote nchini. 

Wakati huo huo, Kiongozi wa Taifa aliwahimza Wakenya kuunga mkono mchakato wa BBI wa marekebisho ya katiba  akisema moango huo unalenga kuafikia Kenya yenye umoja zaidi na maendeleo.

Rais Kenyatta alikamilisha ziara yake ya kikazi kwenye kaunti ya Mombasa kwa kuzindua daraja la kuelea la Liwatoni lenye umbali wa kilomita 1.2 litakalotumika na watu wanaovuka kwa miguu. 

Daraja hilo la baharini la aina ya kipekee katika eneo la Afrika Mashariki litahudumia zaidi wanaovuka kwa miguu kwa kuunganisha eneo la Liwatoni kisiwani Mombasa na Ras Bofu katika eneo la nchi kavu la Likoni. Hii itasaidia kurahisisha huduma ya kuvuka kwenye feri, ambayo imekuwepo tangu 1937, kuhudumia magari na usafirishaji wa mizigo katika kivukio cha Kilindini bila kuvuruga huduma za meli.

Akiwahutubia wakaazi wa eneo hilo waliojitokeza kumpokea, Kiongozi wa Taifa alisema uekezaji mkubwa wa serikali katika muundomsingi huko pwani na kote nchini utafungua uchumi na kubuni nafasi za kazi kwa vijana. 

“Tumekubaliana na mwanakandarasi kwamba kuanzia tarehe 1 mwezi Januari mwaka 2021, daraja hilo litakuwa tayari kwa matumizi ya umma kuvuka hadi au kutoka kisiwani na kuwawezesha kufika mahali pa kazi na nyumbani kwa urahisi badala ya kutegemea kivukio cha Likoni,” kasema Rais.

Wakati huo huo, Rais alionya wakenya dhidi ya wanasiasa wasio wa kweli ambao wanaendelea kupotosha umma na bila maana kuchochea umma kuhusu shughuli za bandari ya Mombasa pamoja na reli ya kisasa ya SGR.

Rais Kenyatta alisema kwamba kinyume na uwongo unaosambazwa na baadhi ya wanasiasa, huduma ya reli ya kisasa pamoja na upanuzi wa bandari umeongeza zaidi biashara za ziada zinazohudumia bandari hiyo kama vile wasafirishaji wa mizigo kwa malori ambao husafirisha zaidi ya asilimia 70 ya shehena inayotoka kwa bandari hiyo na ambayo imekua mno katika miaka ya majuzi.

“Tulipoanza kupanua bandari, kulikuwa na takriban makasha milioni 20 ambayo yalikuwa yamesongamana. Upanuzi wa bandari umeongeza idadi ya makasha na haya yote hayawezi kusafirishwa kwa kutumia SGR. Malori pia yanasafirisha makasha yao kila siku.

“Tusiwe watu wanaowachochea wakenya kwa malengo ya kibinafsi ya kisiasa,” kasema Rais Kenyatta. 

Rais alitaja miradi kadha ya muundomsingi itakayoanzishwa miezi michache ijayo katika eneo la Pwani ikiwemo barabara ya kimataifa kutoka Malindi kupitia Dongo Kundu hadi Lunga Lunga na hatimaye Bagamoyo nchini Tanzania kuunganisha watu wa mataifa haya mawili.

 

Maarufu Zaidi

RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2026. All rights reserved