logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mwanahabari wa KBC auawa kwa kupigwa risasi - Ngong

Mwanahabari wa KBC auawa kwa kupigwa risasi - Ngong

image
na Radio Jambo

Habari08 April 2021 - 06:45

Muhtasari


• Barasa alikuwa amewasili nyumbani kwake mwendo wa saa mbili unusu jioni wakati genge lililokuwa likingojea langoni lililazimisha kuingia ndani

• Kulingana na familia yake, majambazi watatu waliojihami walikuwa wakimsubiri afike.

• Jambazi mmoja alimpiga risasi mbili kichwani kwa karibu sana.

Mwanahabari wa KBC Betty Barasa. Picha: HISANI

Mwandishi wa habari wa KBC Jumatano usiku aliuawa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake mtaani Ngong katika kisa cha wizi.

Betty Barasa, mhariri wa video na mtangazaji huyo wa kitaifa alipigwa risasi katika eneo la Ololua, Ngong.

Barasa alikuwa amewasili nyumbani kwake mwendo wa saa mbili unusu jioni wakati genge lililokuwa likingojea langoni lililazimisha kuingia ndani wakati lango lilipofunguliwa, mashahidi walisema.

 

Alikuwa kazini Jumatano na alikuwa ametoka ofisini katikati mwa jiji la Nairobi kuelekea katika nyumba yake mpya akitarajia kujiunga na mumewe na watoto watatu.

Alikuwa tu amehamia katika nyumba yake mpya siku chache zilizopita.

Kulingana na familia yake, majambazi watatu waliojihami walikuwa wakimsubiri afike.

Wawili kati yao walikuwa wamejihami kwa bunduki za AK47.

Aliendesha gari mpaka kwenye lango na msaidizi wa nyumba alikimbia kuufungua.

Alipokuwa akiingia, watu watatu walijilazimisha kuingia, na mfanyikazi wa nyumba akakimbia kwenye giza akipiga kelele akisema kulikuwa na majambazi ndani ya boma.

Kelele za mfanyikazi hazikuwababaisha waliendelea na shughuli zao.

 

Kulingana na familia, majambazi hao walimfuata Betty hadi mahali alipoegesha gari na kumuamuru atoke awapeleke ndani ya nyumba wakiwa wamemshikia bunduki.

Mumewe na watoto walikuwa ndani ya nyumba, wakiwa na hofu kufuatia mayowe ya msaidizi.

Walioshuhudia walisema mmoja wa majambazi alitaka pesa kutoka kwa Betty na akamwamuru ampeleke kwenye chumba cha kulala ghorofani.

Wengine wawili walibaki sebuleni ambapo watu wengine wa familia walikuwa.

Majambazi waliwasumbua wakidai wapewe pesa na vitu vingine vya thamani.

Mume na watoto waliomba genge hilo liwaachilie na kuchukua chochote walichotaka.

Huku wakibishana sebuleni walisikia milio miwili ya risasi.

Jambazi aliyekuwa ameenda na Betty alikuwa amempiga risasi mbili kichwani kwa karibu sana kwani pia alikuwa amemuomba amuache.

Baada ya kumpiga risasi, genge lilinyakua tarakilishi na simu ya Betty na kuondoka.

Wenyeji ambao walisikia milio ya risasi walikimbia kwenye boma walipogundua kwamba jirani yao alikuwa ameuawa.

Polisi walisema bado hawajakamata au kujua sababu ya mauaji hayo.

Eneo hilo linakua kwa kasi kutokana na kuwepo kwa Reli ya SGR.

Wengi ambao walikuwa wamenunua ardhi katika eneo hilo sasa wanajenga nyumba.

Karibu na nyumba ya Barasa kuna nyumba ambayo bado inaendelea kujengwa na inaaminika genge hilo lilikuwa limejificha hapo kusubiri kuwasili kwake.

Marehemu pia alikuwa akifundisha katika Taasisi ya Mawasiliano ya Kenya (KIMC).


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved