Mansukh Patel, mmiliki wa Shamba la Kahawa la Solai, ambamo kuna Bwawa la Solai lililosababisha vifo vya takriban watu 50 na kuacha mamia bila makao ameaga dunia.
Patel alifariki siku ya Jumatatu jioni mwendo wa saa kumi jini katika Hospitali ya Agha Khan mjini Nairobi alikokuwa akipokea matibabu baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Msimamizi wa Shamba la Solai, Kiragu Maina alisema mfanyibiashara huyo alikuwa nyumbani kwake Nairobi wakati alipoanza kuhisimi maumivu kabla ya kulazwa hospitalini mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema mipango ya mazishi ya mwendazake inaendelea. Mansukh alikuwa akimiliki Kampuni ya Solai Group ambayo ni pamoja na kampuni kubwa na kongwe zaidi ya chumvi ya jikoni Kensalt Limited na Solai Coffee Estates ambayo hupanda maua, macadamia, kahawa na mazao mengine ya bustani kwa kuuzwa nje ya nchi.
"Alikuwa bado ana bidii wakati akiugua na alikuwa akitembelea miradi yake ya biashara nchini Kenya, Afrika na nje ya nchi chini ya Kampuni za Solai Group pf," alisema Maina.
Mansukh hakupenda kujionyesha licha ya kumiliki biashara kubwa hadi mkasa wa Mei 9, 2018 wakati Bwawa kubwa kwenye shamba lake la Patel Coffee Estate huko Solai lilipovunja kingo zake.
Mwanawe, Perry Mansukh alikuwa miongoni mwa watu tisa waliokamatwa na kushtakiwa kwa vifo vya watu 50 kabla ya kuachiliwa huru na Mahakama Kuu huko Naivasha kwa kukosa ushahidi.