logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mbinu maarufu ambazo wasanii wa Kenya hutumia kutafuta kiki

Kwa lugha ya mtaani, kiki ni kitendo cha mtu haswa msanii kuanzisha drama ili kuibua gumzo ama kutaka kuangaziwa zaidi na watu.

image
na Radio Jambo

Habari14 October 2021 - 05:16

Muhtasari


•Kwa lugha ya mtaani, kiki (clout) ni kitendo cha mtu haswa msanii kuanzisha drama ili kuibua gumzo ama kutaka kuangaziwa zaidi na watu.

Je wafahamu kiki ni nini?

Kulingana na Kamusi ya Kiswahili, neno kiki linamaanisha pigo la mpira kwa kutumia mguu.

Kwa lugha ya mtaani, kiki (clout) ni kitendo cha mtu haswa msanii kuanzisha drama ili kuibua gumzo ama kutaka kuangaziwa zaidi na watu.

Wasanii wengi, sio tu nchini Kenya bali kote dunia wanajulikana kutafuta kiki sana haswa wanapotazamia kutoa wimbo mpya ama kufanya tamasha.fulani.

Kunazo mbinu tofauti ambazo hutumika kutafuta kiki na zote hutegemea ubunifu wa anayetafuta kiki.

Hizi hapa baadhi ya mbinu za kawaida ambazo wasanii nchini Kenya wanapendelea kutumia sana:-

1. Mahusiano

Kwa kawaida ndoa ama mahusiano hufanyika kati ya wawili ambao wanapendana na wanatazamia kuanzisha familia pamoja.

Aghalabu watu wanapoamuua kujitosa kwenye mahusiano huwa wanaangaziwa sana na jamii wengi wakitaka kufuatilia mwelekeo wa mahusiano yale.

Hata hivo hapo awali mahusiano yametumika vibaya na baadhi ya wasanii ambao hujifanya kama kwamba wako kwenye mahusiano mradi tu waangaziwe na watu.

Mbinu hii imetumika sana nchini haswa wakati msanii wa kiume anatazamia kushirikiana na msanii wa kike kwenye wimbo.

Nadia Mukami aliwahi kudanganya kwamba ako kwenye mahusiano na jamaa mwenye asili ya Kihindi kisha ikafahamika baadae kuwa alitaka tu kumshirikisha kwa wimbo.

2. Utengano

Wakati kunao wasanii  ambao hujitosa kwenye mahusiano ili kuibua gumzo miongoni mwa watu, kunao wanandoa au wapenzi ambao haumua kujifanya kama kwamba wametengana almradi tu waangaziwe zaidi na watu.

Hii ni jambo la kawaida haswa miongoni mwa wapenzi mashuhuri ambao wanatazamia kufanya mradi pamoja kama vile wimbo ama video.

Mfano mzuri ni wakati mwanamuziki Bahati na mpenzi wake Diana Marua walikuwa wanapanga kutoa wimbo 'mtaachana tu' pamoja walifanya wanamitandao waamini kwamba wametengana.

3. Ugonjwa/Ajali

Kunao wasanii ambao hupita mipaka na kujifanya kama kwamba ni wagonjwa ama wamehusika kwenye ajali ili tu waangaziwe na watu.

Ijapokuwa jambo hili ni la kusikitisha, kunao wasanii ambao kwa kawaida  hawajalishwi na matokeo ya matendo yao bora tu wanase umakini wa watu.

Mbinu hii ya kughadhabisha imetumika na wasanii wengi duniani.

Kuna gumzo mitandaoni kwamba ujumbe wa Willy Paul wa hivi majuzi kwenye mtandao wa Instagram ulioashiria kama kwamba amekabiliwa na msongo wa mawazo huenda ikawa ni kiki tu anatafuta kwani anatazamia kuzindua albamu yake hivi majuzi.

4. Ugomvi

Kunao wasanii ambao hujifanya kama kwamba wanazozana ili tu kuibua gumzo na kuangaziwa na mashabiki wao.

Wasanii hawa hukorofishana hadharani ama mitandaoni  ili kunasa watu kisha baada ya kufanikiwa wanafanya mradi wa sanaa pamoja.

Mfano mzuri wa hivi karibuni ni wakati Willy Paul na Size 8 walijifanya kama kwamba wanazozana kisha wakashirikiana kutoa wimbo 'Lenga' pamoja mnamo mwezi Julai.

5. Kashfa

Kashfa ni jambo la aibu lililofanyika kwa siri ambalo limefichuka.

Kashfa huenda ikawa ya kimapenzi, kingono au ikahusiana na masuala mengine ya maisha.

Kunao wasanii ambao hujifanya kama kwamba wamehusika kwenye kashfa mradi tu wapate kufahamika zaidi ama kuangaziwa na watu.

Kashfa za kawaida miongoni mwa wasanii ni zile ambazo zinahusisha mapenzi, ngono au mitindo ya maisha.

Maarufu Zaidi

RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2026. All rights reserved