Walimu wawili katika kaunti ya Makueni wanaodaiwa kupokea kitita cha shilingi milioni moja kutoka kwa mwanasiasa aliyekuwa amezuru eneo hilo walinusurika kifo baada ya polisi kuwaokoa kutoka kwa kikundi cha waendesha bodaboda waliotaka kuwaangamiza.
Kulingana na Dci, wawili hao ambao ni walimu katika shule ya msingi walikimbia katika kituo cha polisi cha Kambu na kujificha nyuma ya meza ya kupigia ripoti huku kikundi kikubwa cha waendesha bodaboda kikiwa kimewaandama unyo kwa unyo.
Polisi wawili waliokuwa kituoni walipata wakati mgumu kujaribu kuthibiti waendesha bodaboda hao ambao walitaka kupata sehemu ya pesa ambazo walidai walimu wale walikuwa wamepokea.
Iliripotiwa kuwa walimu hao walipopokea pesa zile walikosa kugawia waendesha bodaboda wale pamoja na wanawake waliokuwa wanauza bidhaa sokoni na wakaamua kutoroka nazo zote.
Kufuatia madai hayo waendesha bodaboda wale walianza kuwakimbiza walimu hao wakidai kuwaangamiza kutokana na kile walisema ni kunyang'anywa haki yao.
Waendesha bodaboda wale walianza kutupa vitu mbalimbali kituoni katika jitihada za kuwatoa walimu hao na hapo ikabidi maafisa wa polisi waliokuwepo waombe usaidizi kutoka kwa wenzao katika kituo cha Mtito Andei.
Baada ya idadi ya polisi kuongezeka kikundi kile kiliweza kutawanywa huku uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo uking'oa nanga.