Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho jamaa aliyejitambulisha kama Caleb Baraza kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Peris ambaye alisema walitengana takriban miezi minne iliyopita kutokana na fitina za majirani.
Baraza alisema kwamba ndoa yake ya miaka miwili unusu ilisambaritika baada ya majirani kumchochea kwa mkewe kwamba alikuwa anajihusisha na mipango ya kando.
"Nilikuwa natoka kwenda kuchota maji nao majirani wanaenda kumwambia ti nina mipango ya kando. Siku moja nilipotoka kazini nilipata ameshafunga virago na kwenda nyumbani kwao... sikuwa nanyemelea mahali. Yeye hajawahi kunipata na mwanamke yeyote ama kupata msichana kwa simu. Ijapokuwa kwa simu kulikuwa na namba za wateja wa maji. Hao wateja wakipiga simu walijaribu kuniambia niwapelekee maji mke wangu alikuwa anasema eti ni bibi yangu. Wakati mwingine hata nilikuwa namwachia simu yeye aongee na wao sio eti nilikuwa naficha simu au nini. Hawajawahi kutuma jumbe, walikuwa wanapiga simu tu" Baraza alisimulia.
Baraza alifichua kwamba baada ya kutengana mkewe alimuomba pesa za kugharamia matibabu ya mtoto wao ila akakosa kumtumia kwa kuwa hakuwa nazo. Pia alikiri kwamba alimtumia mkewe maneno mabaya kutokana na hasira.
Peris alipopigiwa simu alimtetesha Baraza kwa kukosa kushughulikia mtoto wao alipokuwa mgonjwa.
Peris alifichua kwamba mumewe alimtesa walipokuwa pamoja.
"Mateso yenye umenipitishia kwenu siwezi rudi. Ulitaka kunidunga na kisu alafu mimi nirudi kwenu. Wewe mwenyewe ndio uliniambia nitoke kwa nyumba yako nikuachie amani, nilitoka nikakuachia, nini ingine unataka? " Peris alisema.
Pia alifichua kwamba mumewe aliwahi kutumia wazazi wake jumbe akiwaita wajinga na wachawi.
"Niliona anachukulia wazazi wangu kuwa wenda wazimu sasa siwezi rudi kwao." Alisema.
Ijapokuwa Peris alikubali kumsamehe Baraza alishikilia msimamo wake kwamba hakuna uwezekano wao kurudiana.