Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli amepuuzilia mbali mahusiano kati yake na Bi Roselinda Simiyu ambaye alijitambulisha kama mke wake Ijumaa alipojiunga na UDA.
Bi Roselinda alizinduliwa kama mwanachama mpya wa UDA katika ziara ya naibu rais ya eneo la Magharibi ambapo alihutubia wakazi na kujitambulisha kama mke wa Atwoli
"Mimi naitwa Mama Roselinda Simiyu. Mzee wangu anaitwa Francis Atwoli na niko ndani, ndani ya Hustler!" Bi Roselinda alisema.
Kufuatia hayo Atwoli alijitosa kwenye mitandaoni ya kijamii na kueleza kuwa walitengana na Bi Roselinda na hamtambui tena kama mwanafamilia wake.
Hali kadhalika bosi wa COTU alisisitiza kwamba eneo la Magharibi linaunga mkono muungano wa Azimio la Umoja huku akipatia Ruto idhini ya kumchukua mke huyo wake wa zamani bila malipo.
"Roselinda alijisalimisha kwa William Ruto mnamo 2007 katika nyumba yake iliyo mjini Eldoret. Hayupo tena kwenye orodha ya jamaa zangu. Ruto sasa anaweza kumuongeza, bila malipo, kwa wake zake wawili wa ndevu aliowapata hivi majuzi ili awe na wake watatu kutoka magharibi. Eneo la Magharibi liko katika Azimio" Atwoli alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Kwa sasa Atwoli ako kwenye ndoa na mtangazaji wa habari wa KTN Mary Kilobi baada ya kutengana na Bi Roselinda miaka kadhaa iliyopita.