logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Roman Abramovich kuiuza Chelsea, mapato kutumika kusaidia wahanga wa vita vya Ukraine

Amesema uamuzi huo ni kwa manufaa ya klabu, mashabiki, wafanyikazi pamoja na wadhamini.

image
na Radio Jambo

Habari03 March 2022 - 03:01

Muhtasari


•Roman amesema kuwa uamuzi huo mgumu ambao amefanya ni kwa manufaa ya klabu, mashabiki, wafanyikazi pamoja na wadhamini na washirika wengine.

•Amesema kuwa mapato yote yatakayotokana na uuzaji wa klabu hiyo yatatumika kusaidia waathiriwa wa vita vinavyoendelea Ukraine.

Mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich

Mmiliki wa Chelsea, bwenyenye  Roman Abramovich kutoka Urusi ametangaza wazi kuwa yuko tayari kuuza klabu hiyo ya London.

Kupitia taarifa iliyotolewa Jumatano, Roman amesema kuwa uamuzi huo mgumu ambao amefanya ni kwa manufaa ya klabu, mashabiki, wafanyikazi pamoja na wadhamini na washirika wengine.

"Kama nilivyosema hapo awali, kila mara nimekuwa nikichukua maamuzi kwa nia njema ya Klabu. Kwa hali ilivyo sasa, nimechukua uamuzi wa kuiuza Chelsea, kwani naamini hii ni kwa manufaa ya Klabu, mashabiki, wafanyakazi, pamoja na wadhamini na washirika wa Klabu. Uuzaji wa Klabu hautaharakishwa bali utafuata taratibu zinazostahili. Sitaomba mkopo wowote ulipwe. Hii haijawahi kuwa kuhusu biashara wala pesa kwangu, lakini kuhusu upendo wa kweli kwa mchezo na Klabu," Abramovich alisema.

Mrusi huyo amesema kuwa mapato yote yatakayotokana na uuzaji wa klabu hiyo yatatumika kusaidia waathiriwa wa vita vinavyoendelea Ukraine.

Roman ambaye alinunua Chelsea takriban miongo miwili iliyopita amesema kuwa huo umekuwa uamuzi mgumu sana kwake kufanya ila licha ya yote klabu hiyo na mashabiki watasalia moyoni mwake.

"Nimeiagiza timu yangu kuanzisha shirika la misaada ambapo mapato yote kutokana na mauzo yatawekwa. Shirika hilo  litakuwa kwa manufaa ya wahasiriwa wote wa vita nchini Ukraine. Hii ni pamoja na kutoa fedha muhimu kwa mahitaji ya dharura na ya haraka ya waathiriwa, pamoja na kusaidia kazi ya muda mrefu ya kufufua uchumi. Tafadhali fahamu kuwa huu umekuwa uamuzi mgumu sana kufanya, na inaniuma sana kuachana na Klabu kwa njia hii. Hata hivyo, ninaamini hii ni kwa manufaa ya Klabu. Natumai kwamba nitaweza kutembelea Stamford Bridge kwa mara ya mwisho ili kuwaaga ninyi nyote ana kwa ana. Imekuwa fursa ya maisha kuwa sehemu ya Chelsea FC na ninajivunia mafanikio yetu yote ya pamoja. Klabu ya Soka ya Chelsea na wafuasi wake daima watakuwa moyoni mwangu." Amesema Roman.

Haya yanajiri huku klabu nyingi za Ulaya zikiendelea kuwafurusha wadhamini na washirika wao kutoka Urusi kufuatia mashambulizi kwa Ukraine.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved