Mmoja wa mabinti wa marehemu Mark Too ambaye alizaliwa nje ya ndoa ameagiza vipimo vya DNA kufanyika ili kuthibitisha dai lake kupatiwa sehemu ya mali ya babake yenye dhamani ya bilioni 7.
Mwanasiasa huyo wa enzi za Moi alifariki mnamo Desemba 31, 2016 na kuacha wajane wawili waliokuwa wamemzalia watoto saba kwa jumla. Alikuwa na watoto wengine wanne nje ya ndoa akiwemo Jepkoech Too ambaye anaagiza vipimo vya DNA.
Siku ya Jumatatu Jepkoech kupitia wakili wake Diana Ndung’u alimweleza hakimu wa Mahakama Kuu Eric Ogolla kwamba wajane wawili wa Too, Mary na Sophie, walikataa kumtambua kama mnufaika wa mali hiyo.
Ogolla alishughulikia kesi hiyo katika Mahakama Kuu ya Eldoret.
"Ili kutatua suala hilo mara moja, mteja wangu anataka mahakama iamuru uchunguzi wa DNA kama njia ya pekee ya kuthibitisha kuwa yeye ni binti wa marehemu Too," Ndung'u alisema.
Jepkoech alisema DNA ingepuuzilia mbali madai ya mamake wa kambo kwamba yeye si binti wa kibaolojia wa mwanasiasa huyo wa zamani.
"Bwana Jaji, njia ya pekee ya kutatua suala hili la uzazi ni wewe kuagiza kipimo cha DNA ili mteja wangu apate mgao wake halali wa mali ya marehemu babake," Ndung'u alisema.
Too alifariki akiwa na umri wa miaka 60 kutokana na mshtuko wa moyo.
Mkewe wa kwanza Mary ana watoto wanne; Elizabeth Chepkoech Too, Moses Kiprotich Too, Jennifer Jebet Too na Daniel Kipchirchir Too.
Sophie ana watoto watatu; Sandra Jerop Too, Kevin Kipkemei Too na Sharon Jepchumba Too.
Watoto waliozaliwa nje ya ndoa ni Jepkoech Too, Ali Kiptarbei Mark Too, Arafat Mohammed Bakari Too na Sammy Waki (marehemu).
Wamewasilisha stakabadhi kortini wakisema kuwa wao ni watoto wa mbunge huyo mteule wa zamani ambaye alihudumu katika nyadhifa nyingi wakati wa utawala wa Moi.
Mary na Sophie ndio wasimamizi wa mali hiyo linalojumuisha mashamba 19 katika kaunti za Nakuru, Uasin Gishu, Nandi na Trans Nzoia. Mali nyingine ni matrela 10, matrekta 10, magari 11 na hisa katika kampuni sita za Chips Blue.
Too pia alipenda biashara kilimo, ufugaji wa mifugo ya maziwa, kilimo cha mahindi na ngano na real estate.
Alikuwa na nyumba za mamilioni ya shilingi katika maeneo ya Muthaiga na Lavington jijini Nairobi, Milimani mjini Nakuru na Elgon View mjini Eldoret.
Hakimu Ogolla aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 28. Wanafamilia wengi walikuwa mahakamani kusikiliza kesi hiyo.