logo

NOW ON AIR

Listen in Live

"Wengi hawana hatia, mnawatesa bure!" Mike Sonko atetea wanabodaboda kufuatia msako mkali unaoendelea

Hata hivyo amewakashifu waliohusika katika tukio la wiki jana.

image
na Radio Jambo

Habari11 March 2022 - 04:39

Muhtasari


•Sonko amesema makosa ya wanabodaboda waliohusika kwenye tukio la wiki jana hayapaswi kupelekea adhabu kwenye sekta yote ya bodaboda.

•Hata hivyo amewakashifu waliohusika katika kunyanyasa mwanamke anayeripotiwa kuwa mwanadiplomasia wa Zimbabwe.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amejitokeza kutetea wahudumu wa bodaboda kufuatia msako mkali unaoendelea kote nchini. 

Mapema wiki hii rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuwa serikali itakuwa kali zaidi kwa sekta ya bodaboda kufuatia tukio la wiki jana ambapo dereva mwanamke alidaiwa kunyanyaswa na kundi  waendesha bodaboda baada ya kuhusika kwenye ajali katika barabara ya Wangari Maathai.

Kufuatia tangazo hilo la rais maafisa wa polisi kote nchini wamekuwa wakiendeleza msako mkali katika juhudi za kuleta nidhamu zaidi kwenye sekta hiyo. 

Sonko amesema makosa ya wanabodaboda waliohusika kwenye tukio la wiki jana hayapaswi kupelekea adhabu kwenye sekta yote ya bodaboda.

Mwanasiasa huyo ambaye mapema wiki hii aliwekewa marufuku ya kuingia Marekani amesema  wengi wa wahudumu wa bodaboda si wahalifu. Hata hivyo amewakashifu waliohusika katika kunyanyasa mwanamke anayeripotiwa kuwa mwanadiplomasia wa Zimbabwe.

"Kwa taarifa tu, huyu ni Hezron Mwenda, mwendesha pikipiki ambaye aligongwa na mwanamke aliyenyanyaswa. Hezron sio mwanabodaboda, bali ni mfanyakazi wa kampuni ya ufuaji nguo inayofanya VIP. Bado tunalaani wakora waliomnyanyasa huyo mama lakini sio wote, wengi wao hawana hatia mnawatesa bure," Sonko aliandika chini ya picha za jamaa anayedaiwa kuhusika kwenye ajali na mwanadiplomasia huyo.

Wahudumu wa bodaboda kutoka maeneo mbalimbali nchini wamelalamikia hatua ya serikali huku baadhi yao wakiandamana katika barabara mbalimbali nchini.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved