Mjukuu wa aliyekuwa rais wapili wa Kenya Daniel Moi sasa amewasilisha ombi kwa mahakama akidai Sh30 milioni za kulipia bili zake.
Collins Kibet Toroitich anaitaka mahakama kuamuru msimamizi wa mali kubwa ya babu yake alipe pesa hizo huku wakisubiri uamuzi wa kesi ya urithi.
Kibet alielekea kortini kumshtakii Zehrabhanu Janmohammed kwa njama ya kumpokonya urithi. Wakili Mwandamizi Janmohammed ndiye msimamizi wa mali kubwa ya Moi.
Kibet aliambia mahakama kuwa babu yake alikuwa na thamani ya zaidi ya Sh300 bilioni.
Kupitia kwa wakili Pearlyne Omamo, Kibet anasema amefilisika na anaishi kwa kutegemea misaada kutoka kwa watu wema.
Katika hati ya kiapo iliyowasilishwa kortini mnamo Aprili 7, Kibet alisema maelekezo ya kesi ya urithi yalipangwa kutokewa Julai 19, wakati ambao anadai ni mbali sana kwa sababu malipo ya bili zake yamechelewa.
"Julai 19 ni mbali sana na kubainisha kuwa kuna makataa ambayo yamekaribia kutoka kwa mwenye nyumba wa zamani wa mwombaji kulipa kodi yake ya Sh200,702 ifikapo Aprili 19," hati ya kiapo inasomeka.
Kibet alisema yeye ni yatima. Baba yake Jonathan Kipkemboi Moi alifariki mwaka wa 2019 baada ya mamake kufariki miaka miwili mapema. Jonathan alikuwa mwana mkubwa wa Moi.
Katika wosia wake, ambao pia uliwasilishwa kortini, Rais Moi aligawa mali yake kwa usawa kati ya wanawe watano na katika kesi ya kifo cha mmoja wao, kama katika kesi ya Jonathan, watoto wao wangepewa urithi.
Wana wa Moi ni pamoja na Jonathan Kipkemboi, Raymond, John Mark, Philip na Gideon.
Kibet anadai, miongoni mwa mambo mengine, hesabu sahihi ya mali na madeni ya Moi na kuondolewa kwa mamlaka aliyopewa wakili Janmohammed kusimamia mali ya Moi.
Janmohamed alipewa mamlaka ya kusimamia mali ya Moi mnamo Oktoba 9, 2020 baada ya kifo cha Rais huyo wa zamani mnamo Februari 4 mwaka huo huo.
Akiwa mwanawe mkubwa wa Jonathan, Kibet anasema ana haki ya kupata zaidi ya bilioni 5.
Kibet anasema ana watoto watatu wa kiume wenye umri wa miaka 24, 21 na 18 ambao analazimika kulipia karo pamoja na ustawi wao. Anasema mkewe Marsha Dee Amario ni mlemavu kutokana na mshtuko wa kifafa unaomsumbua na hivyo kuhitaji uangalizi maalumu ambao anashindwa kumpatia kutokana na matatizo ya kifedha.
Alisema hana uwezo wa kulipa bili zake na hawezi kuhudumia mahitaji ya kimsingi ya wategemezi wake.
“Hakuna sababu yoyote ya msingi kwa mwombaji na washitakiwa wake kuteseka kwa namna wanavyoteseka wakati maslahi yao yameshughulikiwa kwa uwazi katika wosia wa marehemu, na mali za marehemu ziko vizuri na kweli zina uwezo wa kumudu mahitaji ya mwombaji. wa wategemezi wake,” ilisema hati ya kiapo.
Kibet anaitaka mahakama iamuru Janmohammed amlipe Sh20 milioni ili kukidhi mahitaji yake ya matibabu, chakula, mavazi, elimu, usafiri na mahitaji yake mengine.
Pia anamtaka msimamizi wa mirathi kumlipa Sh10 milioni nyingine ili kuanzisha biashara.
"Inaposubiri kupokea mgawo wake kamili katika mirathi hii, mahakama hii tukufu inamuamuru mlalamikiwa kulipa malipo ya kila mwaka ya mkupuo ya Sh30 milioni kwa ajili ya kugharamia shughuli zake za biashara na malimbikizo ya matibabu na chakula, gharama za mavazi, elimu na usafiri na mahitaji mengine,” ilisema hati ya kiapo.
(Utafsiri: Samuel Maina)