logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ruto aongoza kwa 45.5% huku Raila akifuata na 41.3 - Kura ya maoni

Ruto aongoza kwa 45.5% huku Raila akifuata na 41.3 - Kura ya maoni.

image
na Radio Jambo

Habari21 April 2022 - 04:54

Muhtasari


• Kinyang'anyiro cha urais cha Agosti 9 kinaonekana kuuchacha  huku Naibu Rais William Ruto na mgombeaji wa Azimio la Umoja Raila Odinga wakichuana hadi ukingoni.

• "Tuna imani kubwa kwamba mfumo huu wa upigaji kura ni sahihi sana na vilevile una kasi zaidi kuliko upigaji kura wa jadi wa CATI au upigaji kura wa ana kwa ana," alisema Joshua Oluoch.

Naibu rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga

Kinyang'anyiro cha urais cha Agosti 9 kinaonekana kuuchacha  huku Naibu Rais William Ruto na mgombeaji wa Azimio la Umoja Raila Odinga wakichuana hadi ukingoni.

Kura ya maoni ya mwisho ilionyesha Raila akiongoza kwa asilimia ndogo lakini sasa kura ya hivi punde ya Radio Africa inaonyesha Ruto yuko mbele tena akiwa na asilimia 45.5 ikilinganishwa na asilimia 41.3 ya Odinga.

Kura hii ya hivi punde ilitumia teknolojia mpya ya SMS ambayo ilifanyika kati ya Aprili 1 na 13, 2022, huku wahojiwa 4,497 kutoka kaunti zote 47 wakipewa uzito wa kuakisi sajili ya IEBC ya Novemba 2021.

Upeo wa makosa ni asilimia 4.5 na utafiti ulifadhiliwa na kampuni ya Radio Africa.

"Tuna imani kubwa kwamba mfumo huu wa upigaji kura ni sahihi sana na vilevile una kasi zaidi kuliko upigaji kura wa jadi wa CATI au upigaji kura wa ana kwa ana," alisema Joshua Oluoch.

Julai iliyopita Ruto aliongoza kwa asilimia 42.7 ikilinganishwa na asilimia 14.2 ya Raila. Lakini uongozi huo umepunguzwa kasi na mnamo Machi, kura ya maoni ya Radio Africa ilisema Raila alikuwa anaongoza.

Ilisema Raila alikuwa na asilimia 47.4 huku Ruto akiwa na asilimia 43.4 kama mgombeaji urais anayependelewa na waliohojiwa.

Katika muda wa miezi sita iliyopita, Raila na timu ya Azimio wamejitahidi sana kukata uongozi wa Ruto huku wakiungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta na serikali.

Kura za maoni za hivi majuzi zinaonyesha kuwa zitakuwa mbio za farasi wawili mnamo Agosti 9.

Hakuna mgombea mwingine aliyeonyesha ishara ya kutoa upinzani mkali kwa wawili hao katika kura hizo za maoni.

 Ni Musalia Mudavadi aliyepata asilimia 3.0 pekee na Mwangi wa Iria [asilimia 1.0] aliyejiandikisha katika kura ya maoni ya Radio Afrika mnamo Aprili .

Wengine wote walipata asilimia 2.5 pekee kati yao huku asilimia 6.7 ya waliohojiwa wakiwa hawajaamua kuhusu mgombea watakayempigia kura.

Inaaminika kuwa Ruto ndiye mwenye nguvu zaidi katika eneo la North Rift akiwa na asilimia 68.6 na South Rift akiwa na asilimia 58.9.

Lakini pia alionekana kuwa na umaarufu  katika eneo la kati akiwa na asilimia 57.6 na Mashariki ya Juu akiwa na asilimia 61.2.

Raila alitawala Nyanza kwa asilimia 66.5 na kuongoza Magharibi kwa asilimia 44.5 na Kaskazini Mashariki kwa asilimia 53.9. Anaongoza uwanja muhimu wa vita Pwani kwa asilimia 46.1 ikilinganishwa na asilimia 38.8 ya Ruto. Katikati, alimfuata Ruto kwa asilimia 28.5.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved