Maafisa wa upelelezi wanajaribu kubainisha miili miwili ilipatikana kwenye gari lililoibwa lililopatikana likiwa limetupwa Lucky Summer, Nairobi.
Gari hilo lilipatikana likiwa limetupwa katika uwanja wazi huko Gatheca.
Mmiliki wa gari nyeupe aina ya Toyota Vitz (KCH 715Z) alikuwa akifuatilia suala la wizi wa gari katika Kituo cha Polisi cha Lucky Summer siku ya Alhamisi.
Polisi kupitia taarifa walisema mmiliki wa gari kisha alipokea simu kutoka kwa rafiki yake kwamba alikuwa ameona gari kama hilo uwanjani.
"Alikwenda eneo la tukio akiwa ameandamana na maafisa wa polisi na alipofika, alitambua gari hilo kuwa lake ingawa nambari za mbele na za nyuma zilikuwa zimetolewa," polisi walisema.
Walipochungulia madirishani, polisi waligundua wanaume wawili wa makamo ndani wakiwa na harufu mbaya iliyokuwa ikitoka kwenye gari.
Miili hiyo ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City ikisubiri kutambuliwa na uchunguzi wa maiti ili kubaini chanzo cha kifo hicho.
