Sekta ya uchukuzi imezindua mbinu mpya ya kuwanasa wale wasiozingatia sheria zilizowekwa barabarani.
Washikadau katika mkutano uliofanyika KICC, walipongeza Polisi wa trafiki kwa kazi nzuri ya kuhakikisha kuwa Wakenya wapo salama wanapotumia barabara kwa kuhakikisha wanazingatia sheria za trafiki.
''Ningependa kuongeza kwamba kando na Polisi na wamiliki wa magari kuhakikisha wanatumia barabara vizuri, tunahitaji pia kuhusisha teknolojia ya kisasa kwa madhumuni ya utekelezaji wa sheria za trafiki,'' Oginga alisema.
Mhandisi huyo alisema kuwa kuna majaribio ambayo yamefanyika hapa nchini kwenye barabara ya magharibi ya Outering ambapo teknolojia hizo almaarufu E Police zimeanza kutumika.
''E Police inauwezo wakunasa gari kwenye kamera ukiwa unatumia barabara vibaya na kusambaza taarifa hizo kwa kituo cha usimamizi wa trafiki na kwa hilo utashtakiwa kwa kosa hilo'' aliongeza.
Alisema kuwa wanatazamia kuweka mfumo huo katika barabara zote ili kusaidia katika kudhibiti sheria za usafiri ambao umekuwa tatizo kubwa nchini.
''Pia kutawekwa vidhibiti mwendokasi barabarani ili kuepusha suala la maafisa kutoka NTSA kujificha kwenye kichaka kupima ukomo wa mwendo kasi wa magari mbalimbali'' Oginga alisema.
Teknolojia hiyo mpya itaweza kutambua usajili wa magari na kumuonya dereva juu ya mwendokasi ili utakapokamatwa na Polisi hatakuwa na malalamishui kwa kuwa alishapewa tahadhari mapema na mfumo hiyo mpya.