logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Afisa wa polisi atoroka baada ya kumbaka mfungwa kwenye seli

"Alimwomba mshukiwa aliyekuwa amevalia suruali yake ya jeans kuandamana naye kwani afisa mkuu wa kituo alitaka kuzungumza naye," OCPD alisema.

image
na

Habari20 July 2022 - 08:12

Muhtasari


• Mfungwa huyo mwanamke alikuwa ameshikiliwa kituoni hapo kwa tuhuma za wizi wa watoto kinyume na sheria.

• Polisi huyo aliingia kwenye seli ya kike na kumuamrisha amfuate ambapo alimpeleka kwenye chumba kimoja na kumuamrisha kuvua nguo akimuwekea mtutu wa bunduki.

Polisi mmoja katika kaunti ya Nandi anasakwa kwa tuhuma za kumbaka mfungwa kwenye seli ya kituo cha polisi cha Kaimosi.

Inadaiwa polisi huyo alimlazimisha kwa mtutu wa bunduki mwakamke huyo mfungwa kwenye kituo hicho kabla ya kumtendea unyama.

Mfungwa huyo alikuwa ametiwa kwenye seli kwa tuhuma za wizi wa watoto na alikuwa anasubiria kupandishwa kizimbani kabla unyama huo kumtendekea.

Samuel Wanyonyi, 31, alikuwa afisa wa zamu akisimamia dawati la ripoti katika kituo cha polisi alipodaiwa kutekeleza kosa hilo.

OCPD wa kati wa Nandi Doris Chemos alisema afisa huyo aliyejihami kwa bunduki aliingia kwenye seli ya wanawake na kumchukua mwanamke huyo ambaye alikuwa miongoni mwa washukiwa wanne waliokuwa wakizuiliwa.

"Alimwomba mshukiwa aliyekuwa amevalia suruali yake ya jeans kuandamana naye kwani afisa mkuu wa kituo alitaka kuzungumza naye," OCPD alisema.

Bila kujua kilichokuwa mbele yake, mshukiwa huyo aliyegeuka kuwa mwathirika alimfuata afisa huyo mwenye silaha na kumuingiza kwenye chumba kingine kilichokuwa tupu ndani ya kituo cha polisi ambapo alimuamuru avue nguo zake kwa mtutu wa bunduki.

Kisha alimbaka mwanamke huyo katika chumba cha kutolea taarifa kisha akamsindikiza hadi kwenye seli akitishia kumuua iwapo angefichua tukio la ubakaji.

"Leo asubuhi, wakati wa ukaguzi wa kawaida, OCS alikabiliwa na mwanamke huyo na kumjulisha kile afisa wa zamu ya usiku alikuwa amemfanyia," Chemos alisema.

Ni baada ya ripoti hiyo ambapo polisi walichukua hatua ya kumpeleka mwanamke huyo hospitalini kwa uchunguzi.

Fomu ya P3 ilitolewa na kujazwa na daktari na mwathiriwa katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Kapsabet.

Alipogundua kuwa kisa hicho kilikuwa kimeripotiwa, afisa huyo ambaye alikuwa akitayarisha kifungua kinywa chake katika makao ya polisi alijitosa kwenye shamba la mahindi lililokuwa karibu na kutoweka.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved