logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Uchunguzi wa maiti umeshindwa kubaini jinsi afisa wa IEBC Daniel Musyoka alifariki

"Hatuwezi kubaini chanzo cha kifo. Hakuna majeraha ya mwili yanayoonyesha chanzo cha kifo. Tumekusanya sampuli kutoka kwa mwili huo kwa uchunguzi zaidi wa kitaalamu katika maabara ya serikali," alisema Dkt Njeru.

image
na Radio Jambo

Habari18 August 2022 - 10:05

Muhtasari


• Viungo vingi vya ndani vya Musyoka vilipatikana vikiwa bila madhara yoyote yanayoweka kuonesha matokeo ya kuuawa kwa kunyongwa

Daniel Musyoka

Baada ya kutoweka wa afisa msimamizi wa uchaguzi katika eneo bunge la Embakasi East Daniel Musyoka, siku chache baadae mwili wake ulipatikana katika hospitali ya kaunti ndogo ya Loitokitok.

Kifo chake kimezua mijadala kinzani katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari huku fumbo kubwa likiwa kubaini mtu aliyetekeleza mauaji hayo ambapo mwili ulipatikana zaidi ya kilomita 200 kutoka eneo alikotoweka.

Kiza kinachozingira mauaji yake kimechukua tena mkondo mwingine tofauti na vifo vya kawaida baada ya wanapatholojia kushindwa kubaini kiini cha kifo chake baada ya upasuaji wa mwili wa Musyoka.

Wataalamu wa magonjwa wanaowakilisha mashirika ya familia na haki za binadamu wakiongozwa na mwanapatholojia wa serikali Dkt Dorothy Njeru, Jumatano walifanya zoezi la upasuaji la saa nne na kufikia hitimisho kwamba hawakuweza kubaini moja kwa moja chanzo cha kifo.

Kulingana na taarifa zilizochapishwa kwenye jarida moja la humu nchini, mwanapatholojia aliyekuwa anasimamia mchakato huo aliwataarifu wanafamilia waliokuwa wamejawa na simanzi na kuchanganyikiwa nje ya makafani, Dkt Njeru alisema mauaji hayo yalifanywa kwa njia "ya kitaalamu" kiasi kwamba hawakuwa na majeraha ya kimwili kuashiria chanzo cha kifo hicho.

Viungo vingi vya ndani vya Musyoka vilipatikana vikiwa bila madhara yoyote yanayoweka kuonesha matokeo ya kuuawa kwa kunyongwa au hata kupigwa kwa kifaa butu au kulishwa sumu.

"Hatuwezi kubaini chanzo cha kifo. Hakuna majeraha ya mwili yanayoonyesha chanzo cha kifo. Tumekusanya sampuli kutoka kwa mwili huo kwa uchunguzi zaidi wa kitaalamu katika maabara ya serikali," alisema Dkt Njeru.

Musyoka alitoweka kwenye kituo chake cha kazi mnamo Agosti 12, zaidi ya kilomita 200 kutoka mahali ambapo mwili wake ulipatikana.  Mwili ulikuwa uchi lakini nguo zake zikiwemo Shuka ya kimasai zilikutwa pembezoni mwa bonde hilo.

Pia kulikuwa na dalili zinazoonekana za mapambano na mateso kabla ya kifo chake. Hakukuwa na hati za utambulisho zilizopatikana kutoka eneo la tukio.

Mauaji ya Musyoka yanafuatiwa na taarifa ya mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati ambaye Jumatano alitoa taarifa ya kuairisha tena chaguzi za ugavana katika kaunti za Mombasa na Kakamega kwa kile alisema kwamba ni kutokuwa na usalama wa kutosha kwa maafisa watakaosimamia uchaguzi huo.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved