Rais William Ruto Jumapili jioni aliwasili Tanzania kwa ziara nyingine ya kiserikali ya siku mbili katika nchi hiyo jirani.
Ziara ya rais ya Tanzania inajiri baada ya kulala nchini Uganda siku ya Jumamosi ambapo alisherehekea Sikukuu ya Uhuru wa nchi hiyo mnamo Jumapili.
Baada ya kumaliza ziara ya Uganda moja kwa moja rais alielekea Tanzania.
Rais anatarajiwa kufanya mazungumzo baina ya nchi hizo mbili na mwenyeji wake rais Samia Suluhu kuhusu masuala yanayohusu mataifa hayo mawili.
Ziara hizo zinaonekana kama sehemu ya juhudi za Ruto kujifahamisha na wenzao wa nchi hiyo jirani huku akianzisha muhula wake kama Rais wa tano wa Kenya.
Ruto ni miongoni mwa viongozi kutoka mataifa mbalimbali walioungana na mamilioni ya raia wa Uganda walioadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa taifa hilo siku ya Jumapili.
Akizungumza Jumapili katika sherehe za maadhimisho hayo zilizofanyika katika uwanja wa Kololo na kupambwa na gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama vya Uganda, Ruto alihimiza ushirikiano zaidi wa nchi za Afrika Mashariki, akimtaka Rais Museveni kuongoza hilo.
'Tunaweza kutengeneza ustawi na kuunganisha fursa katika nchi zetu kwa faida ya watu milioni 300 Afrika mashariki na watu bilioni 1.2 katika bara la Afrika', alisema Ruto.
Kabla ya kumkaribisha Ruto, Rais Museveni katika hotuba yake ya kurasa 30, na yeye alihimiza umuhimu wa kuunganisha nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, ili kujenga uchumi imara.
Alisisitiza pia kuendelea na ujenzi wa bomba la mafuta linalounganisha Uganda na Tanzania, licha ya Umoja wa Ulaya kukosoa ujenzi wake kwa sababu za mazingira.
Mbali na Ruto, viongozi wengine waliohudhuria sherehe hizo za miaka 60 ya uhuru wa Uganda ni pamoja na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit, Rais wa Somalia Hamad Sheikh Muhamud, Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi aliyemuwakilisha Rais Samia Suluhu wa Tanzania na wawakilishi wengine kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo DRC, Mali na Rwanda.
