Viongozi wa chama cha Jubilee kaunti ya Nairobi wametishia kuhakikisha chama hicho kinaondoka katika muungano wa Azimio la Umoja One Kenya katika siku 14 zijazo.
Katika video moja ambayo ilipakiwa kweney mitandao ya kijamii, mwenyekiti wa chama hicho tawi la Nairobi Mark Ndung’u alisema kuwa mipango kabambe ingalipo kuhakiisha Jubilee wanapata talaka yako na kujitenga na Azimio la Umoja.
Alisema kuwa tayari wamekusanya zaidi ya saini elfu 10 kutoka watu wa Nairobi ili kuwezeshqa mchakato wa kuondoka katika muungano huo imefaulu kwa haraka mno.
“Nataka tuwaambie chama chetu cha Jubilee, tumekusanya zaidi ya saini elfu 10 na tunataka tuhakikishe ndani ya siku 14 tumejing’oa kabisa na kuvunja uhusiano na Azimio,” Ndugng’u alisema.
Alitoa sababu kadhaa za kuvunja uchumba wao na Azimio huku akisema chama cha ODM ambacho ni moja ya vyama vingi vilivyounda muungano huo kimekuwa kikiwazunguka na kufanya maamuzi ya kujifaidi wenyewe.
“Mliona tukifanay kura watu wa ODM ambao wanajifanya ndio Azimio peke yao, hata hawakusemezana na Jubilee walikuwa wanafanya maamuzi yao wenyewe. Jambo lingine, ule mkataba wa kuunda Azimio wameficha hatujawahi kuuona, na hatujui ni nini walisaini. Sisi kama Jubilee tunawaambia katika siku 14 mkuwe na mkakati wa kweli sisi tuondoke katika Azimio,” Ndung’u alisema kwa sauti ya mamlaka.
Viongozi hao pia walituhumu ODM kwa kukiuka mikataba ambayo iliwekwa akitolea mfano jinsi Nairobi walipoteza nafasi ya uspika hata baada ya kuwepo kwa maelewano. Kugeukiwa huko pia walisema kulifanyika hata katika bunge la kitaifa ambapo viongozi wa Jubilee wamekuwa wakinyimwa nafasi katika kamati mbalimbali na badala yake kupewa ODM.