Msanii Faustina Charles almaarufu Nandy kutoka Bongo amewacharukia baadhi ya mashabiki wake ambao kila mara wanamganda kama ruba kisa kutaka kujua hali ya mtoto wake na Billnass.
Msanii huyo katika ujumbe mrefu ambao aliuandika Instagram alionekana kuchukia maswali kama hayo huku akiwaambia mashabiki zake kukoma kuchokonoa mambo ya kifamilia bali wabaki tu kwenye mstari wao wa kuwa mashabiki na kusapoti kazi za Sanaa tu basi.
Nandy alisema kuwa si mara ya kwanza anaulizwa iwapo mtoto wake anafurahia ukaribu wake na kunyonya saa ngapi kutokana na mishe zake nyingi ambapo hajawahi onekana hata mara moja na mwanawe.
Aliwatoa wasiwasi kwa kujibu kuwa mtoto wake ako naye muda mwingi tu kila anapoenda sema hajataka kumuonesha hadharani kwa mapaparazi na wapiga picha. Alisema kuwa mwanawe anafurahia kampano yake muda wote na anafurahia maziwa ya mama mpaka ziwa analiacha mwenyewe.
“Hili swala kila nikipost watu wanauliza mtoto yuko wapi? Mara mtoto ananyonya saa ngapi? Jamani hivi mnahisi mambo ya familia ni maigizo au nimezaa fasheni? Mtoto wangu nipo naye kila muda na anapata malezi yote kwa wazazi kama watoto wengine kwa wazazi wao,” Nandy alifoka.
Aliwataka mashabiki zake kuona utofauti kati ya maisha ya uhalisia na yale ya mitandaoni huku akisema kuwa wakianza kufuatilia maisha ya mitandaoni na kufikiri ni ya uhalisia, basi watakuwa hata robo ya maisha yake hawajayajua.
“Msichanganye maisha ya Insta na maisha ya ndoa na yale ya Uhalisia. Huku Insta maisha yangu hata robo hayajafika. Popote nilipo na mtoto wangu yupo, ananyonya mpaka anakataa ziwa mwenyewe, ansshinda na mimi mpaka nikitokea anasikia sauti anaruka kama kichaa. Tuendelee kusapoti muziki mambo ya kifamilia achene niyafurahie faraghani,” Nandy alisema.
