Shule moja ya serikali nchini Uganda ilishuhudia kioja baada ya shule kufunguliwa na mwalimu mkuu wa awali kufika na kumkuta mwalimu mkuu mwingine aliyetumwa hapo kuchukua nafasi yake.
Shule hiyo ya Kabaale iliyoko wilaya ya Namutumba ilikumbwa na msukosuko baada ya mwalimu mkuu wa awali kukataa uhamisho na hivyo kulazimika kuwa na walimu wakuu wawili – kila mmoja akidai ndiye mwalimu mkuu wa shule hiyo ya serikali.
Bwana Fred Kagoye Samanya, mwalimu mkuu huyu wa awali, alikataa uhamisho wa kwenda Shule ya Sekondari ya Nakalama wilayani Iganga. Kwa upande mwingine, Bw Stephen Mutono, mwalimu mkuu mpya aliripoti kazini mnamo Februari 6, kulingana na vyanzo kutoka shuleni, jarida la Uganda liliripoti.
Jarida hilo iliripoti kuwa chanzo cha Samanya kuhamishwa hakijulikani ila wanakijiji walihisi ni kutokana na msururu wa matokeo duni katika mitihani ya kitaifa.
Hali hyoi ilisababisha mamlaka zikiongozwa na Mkuu wa Wilaya, na uongozi wa polisi kuitisha mkutano na kutatua mkanganyiko huo.
Mkutano huo ulilenga kusuluhisha mivutano kati ya wazazi na baadhi ya wafanyikazi ambao wametishia kuweka vifaa chini ikiwa Bw Samanya hataondoka shuleni.
Baadhi walisema kwamba mwalimu mkuu wa kwanza hataki uhamisho kwa sababu anaacha shamba kubwa la mifugo aliloanzisha.
