Aliyekuwa mgombea urais Reuben Kigame amewataka na kuwasihi Wakenya kutowahukumu wengine kupitia mihemko.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter siku ya Jumanne, Kigame alieleza kuwa watu wa LGBTQ wanapaswa kusikilizwa na kueleweka.
"Kwenye LGBTQ, hisia zimepanda kwa sababu hatusikilizani au kuelewana. Matokeo yake, tunahukumu kila mmoja kwa kutumia hisia. Hii haifai kuwa,” Kigame alisema.
"Kusikiliza na kusoma kwa uangalifu ni muhimu kama kuzungumza au kuandika."
Kigame alisema watu wenye ulemavu au matatizo ya kimwili hawapaswi kuhukumiwa au kulaaniwa.
"Hakuna mtu anayepaswa kumhukumu au kulaani mwingine kwa mofolojia, jinsia, maumbile, ulemavu au changamoto ya kimwili," Kigame alisema.
“Ibara ya 27 ya Katiba yetu inathibitisha hili. Walakini, haki yoyote inaweza kupunguzwa na kile tunachofanya nayo. Hata uhuru wa kujumuika umetumiwa vibaya.”
Alisema ni makosa kuwalazimisha vijana kujiunga na LGBTQ kupitia bunge au vishawishi vya kifedha.
"Ni makosa sawa kumlazimisha mtu kubadili dini na kuwa Mkristo au Uislamu kama ilivyo kuwasukuma vijana wetu kujiunga na LGBTQ kwa sheria au motisha za kifedha," alisema.
Matamshi yake yanajiri siku chache baada ya mahakama kutoa uamuzi kuwa wanachama wa LGBTQ wana haki ya kujumuika.
Uamuzi wa mahakama ulipokelewa tofauti kutoka mashirika tofauti huku wengi wakikashifu uamuzi huo.