logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Raila ajibu madai kuwa anataka 'handshake' na rais Ruto

Raila alisema madai hayo hayana msingi, akiyataja kuwa tusi kwa Wakenya.

image
na Radio Jambo

Habari24 March 2023 - 05:09

Muhtasari


•Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema zaidi kwamba hakuna njia yoyote ya kusalimiana na serikali isiyo halali.

•Raila alimshutumu Ruto kwa kujaribu kurudisha nchi kwenye siku za giza za tawala zilizopita.

akiwahutubia wafuasi wake.

Kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga amejibu madai ya baadhi ya viongozi wa Kenya Kwanza wanaomshutumu kwa kutafuta ‘handshake’ (salamu) na Rais William Ruto.

Akizungumza siku ya Alhamisi, Raila alisema madai hayo hayana msingi, akiyataja kuwa tusi kwa Wakenya.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema zaidi kwamba hakuna njia yoyote ya kusalimiana na serikali isiyo halali.

"Kenya Kwanza imeendelea kudai kuwa tunachotafuta ni salamu tu. Tunakanusha vikali uvumi huu usio na msingi kwamba tunaandamana ili kuboresha maisha ya Wakenya kwa sababu tunataka kusalimiana. Hii ni dharau kwa maarifa ya Wakenya, hatuwezi na hatutashiriki kusalimiana na serikali isiyo halali," Raila alisema.

Aliendelea kumshutumu Ruto kwa kujaribu kurudisha nchi kwenye siku za giza za tawala zilizopita.

Raila alisema muungano wa Azimio hautaruhusu hilo kutokea.

"Sisi katika Azimio hatutaruhusu na hatuwezi kumruhusu Ruto atupeleke kwenye siku za giza za jana."

Upinzani bado unasisitiza kwamba Raila alishinda uchaguzi wa urais wa Agosti 2022.

Hata hivyo, Rais Ruto pia anasisitiza kuwa hakutakuwa na kusalimiana na upinzani na kwamba mazungumzo yoyote yatafanyika tu kupitia njia rasmi, likiwemo Bunge.

Viongozi wanaomuunga mkono Ruto wamekuwa wakimkashifu Raila kutokana na maandamano yake dhidi ya serikali.

Wanadai kuwa Raila anatumia tu maandamano kumsokota mkuu wa nchi katika kusalimiana.

Katibu Mkuu wa UDA, Cleophas Malala alidai kuwa baadhi ya watu wa Azimio huanzisha mazungumzo ya kusalimiana na serikali nyakati za usiku.

"Anachofanya Azimio ni njia ya kutaka kusalimiana na Ruto. Hadi jana jioni walikuwa wakituma watu kuona ikiwa wanaweza kuzungumza na Rais wetu," alisema.

Alisema maandamano ya upinzani hayaathiri watu wa Nairobi pekee bali pia sekta mbalimbali zinazoleta fedha nchini.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved