East Africa Specter Limited, kiwanda cha gesi kinachoaminika kumilikiwa na kiongozi wa Azimio Raila Odinga, kilishambuliwa Jumatatu baada ya watu wasiojulikana kupiga mawe sehemu ya mali hiyo.
Katika video inayosambaa mitandaoni madirisha kadhaa yalivunjwa na mawe yaliyotapakaa lango la kiwanda hicho.
Kanda nyingine ya CCTV inaonyesha idadi ya watu takriban 20 wakirusha mawe nje ya lango.
Meneja wa ulinzi na usalama katika kampuni hiyo Humphrey Waswa alisema kuwa watu hao walifika eneo hilo wakiwa na pikipiki na kuanza kurusha mawe kwa takriban dakika 30 kabla ya askari polisi kufika na kuwatawanya watu hao.
"Walikuwa wakisaidiwa na magari manne yasiyokuwa na alama (land cruiser) na tunashuku lengo lao lilikuwa ni Mkurugenzi Mkuu wetu kwa sababu ofisi yake imeharibiwa zaidi," alisema.
Uchunguzi zaidi kuhusu suala hilo unaendelea.
