logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Chelsea wampiga kalamu kocha Graham Potter kufuatia matokeo duni

"Graham amekubali kushirikiana na klabu kuwezesha mabadiliko mazuri," taarifa ilisoma.

image
na Radio Jambo

Habari03 April 2023 - 03:48

Muhtasari


•The Blues walitangaza kwamba mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 47 alikubali kuondoka katika klabu hiyo. 

•Bruno Saltor atachukua usukani wa The Blues kama Kocha Mkuu wa Muda hadi meneja mpya atakapopatikana.

Klabu ya Chelsea imemfuta kazi kocha wake mkuu Graham Potter takriban miezi saba tu baada ya kujiunga nao. Hii ni kufuatia msururu wa matokeo hafifu ambayo klabu hiyo ya London imekuwa ikiandikisha katika wiki za hivi majuzi.

Katika taarifa yao ya Jumapili jioni, The Blues walitangaza kwamba mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 47 alikubali kuondoka katika klabu hiyo. 

"Graham amekubali kushirikiana na klabu kuwezesha mabadiliko mazuri," taarifa ya klabu hiyo ilisoma.

Potter alijiunga na klabu hiyo ya London mwezi Septemba, mwaka jana baada ya kutimuliwa kwa Mjerumani Thomas Tuchel. Miongoni mwa mafanikio yake machache ni kwamba ameiwezesha klabu hiyo kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini kwa upande mwingine ameiacha katika nafasi ya 11 kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza zikiwa zimesalia takriban mechi 10 tu.

"Chelsea ingependa kumshukuru Graham kwa juhudi na mchango wake wote na kumtakia heri kwa siku zijazo," taarifa ilisoma.

Bruno Saltor atachukua usukani wa The Blues kama Kocha Mkuu wa Muda hadi meneja mpya atakapopatikana.

Hatua ya kutimuliwa kwa Potter ilijiri siku moja tu baada ya Chelsea kupoteza kwa klabu ya Aston Villa 2-0. Kwa sasa The Blues wamekalia nafasi ya 11 katika EPL huku wakiwa wamejizolea pointi 38 baada ya mechi 28.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved