Waziri wa vijana na michezo Ababu Namwamba na familia yake Ijumaa Aprili 28 waliandaa misa ya kuhitimisha kipindi cha maombolezo ambacho kwa kawaida huwa ni siku 40.
Namwamba alipakia video ya ibada ya wafu iliyofanyika siku 40 zilizopita katika kanisa la Consolata jijini Nairobi kwa aliyekuwa mama wa watoto wake Priscah Mwaro ambaye aliripotiwa kufa ghafla.
CS alitumia akaunti yake ya Twitter kushiriki wakati wa kukumbukwa yeye na familia yake, wakisherehekea siku 40 ambazo kitamaduni na kidini pia ni kipindi cha kuonesha kukubaliana na matakwa ya Mungu na kuhitimisha rasmi kipindi cha maombolezo.
Katika klipu hiyo, Namwamba na mmoja wa wanawe walikuwa wameketi kando huku wakitamba na mavazi yanayolingana.
Kijana huyo alitafuta faraja kwa baba yake walipokumbatiana kwa nguvu wakati mmoja.
Katika ibada hiyo, picha ya Priscah na baadhi ya maua viliwekwa karibu na padre aliyeongoza ibada ya ukumbusho.
CS Namwamba aliandika: "Pumziko la milele umpe Priscah, ee Bwana. Na mwanga wa milele umuangazie. Roho ya waaminifu iondoke kwa rehema za Mungu ipumzike kwa amani. Amina."
Mke wa zamani wa Waziri Namwamba alizikwa nyumbani kwake Budalangi, Kaunti ya Busia, Machi 18. Mnamo Machi 17, Namwamba, marafiki, na familia walimfanyia misa katika Consolata Shrine huko Westlands, Nairobi.
Kipindi hicho, Radio Jambo tuliripoti jinsi Namwamba alivyomiminiwa hongera na wakenya wengi baada ya kukubali kumzika Mwaro katika boma lake licha ya kwamba walikuwa wameachana.
