logo

NOW ON AIR

Listen in Live

"Mkisia nimekufa, yameniuwa!" Harmonize tayari kuuawa na mahaba ya mpenzi wake mpya

Konde Boy ameendelea kudokeza kuwa amezama kabisa katika dimbwi la mahaba.

image
na Radio Jambo

Habari06 June 2023 - 04:47

Muhtasari


•Siku ya Jumanne asubuhi, bosi huyo wa lebo ya Konde Music Worldwide alibainisha kwamba yupo tayari kuuawa na mapenzi.

•"Acha nife kama nguli 2pac. Mkisikia nimekufa, yameniuwa," alisema.

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ameendelea kudokeza kuwa amezama kabisa katika dimbwi la mahaba.

Siku ya Jumanne asubuhi, bosi huyo wa lebo ya Konde Music Worldwide alibainisha kwamba yupo tayari kuuawa na mapenzi.

"Udhaifu wangu wa kupenda, ni kupenda kile ambacho kinakaribia kuniua," Harmonize alisema kwenye mtandao wa Instagram.

Konde Boy aliambatanisha ujumbe wake na video iliyoonyesha picha ya ukutani ya mwimbaji nguli wa hiphop, marehemu 2pac Shakur ambaye anadaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi mwaka wa 1996.

"Acha nife kama nguli 2pac. Mkisikia nimekufa, yameniuwa," alisema.

Kauli ya staa huyo wa Bongo inakuja siku chache tu kabla ya ziara yake ya muziki nchini Australia. Ameratibiwa kutumbuiza katika miji ya Sydney, Adelaide, Perth na Melbourne  mnamo Juni 9, 10, 11 na 16 mtawalia.

Mwezi uliopita, alieleza wasiwasi wake kuhusu ziara yake ya Australia akibainisha kuwa ni nchi ya aliyekuwa mpenziwe, Briana Jai.

Kufuatia hayo, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alimuomba Mungu aingilie kati ziara hiyo isilete matatizo katika mahusiano yake.

"Australia ni mahali atokako Brianna!! Mungu anilinde na penzi changu hii safari isije kuwa mwanzo wa matatizo," Konde Boy alisema.

Aliongeza "Juni 9 Sydney, Juni 10 Adelaide, Juni 11 Perth, Juni 16 Melbourne, kateni tiketi zenu naja."

Hata hivyo hakufichua iwapo ana mpango wa kukutana na mrembo huyo wa Australia ambaye aliachana naye mwaka jana.

Harmonize alitangaza kutengana na Briana Machi mwaka jana kabla ya kuanza juhudi za kufufua uhusiano wake na Kajala.

Takriban mwezi mmoja uliopita, alimtambulisha mrembo wa Rwanda Phiona almaarufu Yolo the Queen kama mpenzi wake mpya.

"Sawa, siko single tena nimechukuliwa tayari," alisema.

Konde Boy alidokeza amemfahamu Phiona kwa miaka minne iliyopita akitaja kuwa ni wakati mwafaka wa kujaribu mahusiano.

Huku akionekana kuwatupia vijembe wapenzi wake wa zamani k.m Kajala Masanja, Wolper na Sarah Michelloti, alibainisha kuwa mwanasosholaiti huyo wa Rwanda ni zaidi ya wanawake wote ambao aliwahi kuchumbiana nao.

"Naona ni wakati wa kukuonyesha jinsi nilivyo mwanaume wa kweli. Nakupenda sana Yolo The Queen. Umepita kila msichana niliyekutana naye maishani mwangu. Umenifanya hata nijisikie kuwa mimi ni Mnyarwanda," alisema.

Aliendelea kudokeza kwamba hata anapanga kununua nyumba nchini Rwanda ili mradi tu kuwa karibu na mpenzi wake mpya.

Ili kuthibisha mapenzi yake kwa mlimbwende huyo, staa huyo wa bongo fleva alidokeza kwamba anapanga kuchorwa tattoo yake ambayo kulingana naye, itakuwa ya mwisho kabisa kuchorwa mwili mwake.

"Sawa, napata tattoo yangu ya mwisho. Sitokuja choraga tena. Bila shaka ni ya uso wako mzuri Phiona," alisema.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved