TikToker Kelvin Kinuthia amefichua kwa nini anapenda kuvaa mavazi ya kike yanayokinzana na jinsia yake ya kiume.
Katika mahojiano na mwanablogu Oga Obinna, Kinuthia alisema kuwa kuvaa mavazi ya kike hali ya kuwa yeye ni mwanamume si jambo kubwa linaloweza kuwanyima watu usingizi kwani ni mtindo wake wa fasheni ambao haufai kukosolewa na yeyote.
Mkuza maudhui huyo ambaye hivi majuzi amenunua gari lake la kwanza kutokana na juhudi zake za kuwafurahisha mashabiki wake kwa kuvalia mavazi ya kike, alisema kuwa yeye anapenda nguo fupi fupi tu.
Kila anapovalia mavazi mafupi, Kinuthia alisema hupata ujasiri mkubwa na himizo la kukaa jinsi anavyotaka bila kujali wanachosema walimwengu.
“Mimi napenda rinda fupi, ama suruali. Zile fupi fupi tu hunipunga kweli kweli. Ni vitu tu vya kawaida na ningependa kuwaambia watu kuvaa nguo kinyume na maumbile yako si vibaya, watu waendelee kuvaa. Kuwa wewe mwenyewe. Kuwa wewe na furahia maisha,” Kinuthia alishauri.
Kinuthia alikanusha madai ya kuvaa mavazi ya ndani ya wanawake kama Thong, akisisitiza kwamba yeye hufurahia tu kuvalia rinda au suruali za kike zile fupi peke yake.
Kinuthia alinunua gari lake la kwanza mwishoni mwa juma la kuwashangaza wengi alipolitambulisha kama mtoto wake kwa jina Blessing.
Wiki kadhaa zilizopita, Kinuthia alisema kwamba alikuwa anatarajia mtoto na wengi walibaki vinywa wazi kusikia hivyo, kumbe ujio wa gari lake ndio alikuwa amewaaminisha watu kama mtoto.