Msanii wa Bongo Fleva ambaye anafanya vizuri kwenye Bongo Fleva, Jay Melody amefichua sababu ambayo imemfanya mpaka sasa licha ya kujijengea jina kubwa hajakurupukia mienendo na mitindo ya kisasa ambayo wasanii wengi huonesha pindi jina linapokuwa kubwa kwenye tasnia.
Msanii huyo ambaye anajiandaa kwa ajili ya tamasha lake la kutumbuiza na live band alisema kwamba yeye amechagua njia tofauti kidogo kwa sababu anataka kudumu kwenye muziki kwa muda mrefu.
Jay Melody alisema kwamba hawezi jiingiza katika mienendo kama ya kubadilisha wanawake tofauti kimapenzi, kujichora tattoo na kuvaa mavazi mengine ya kustaajabisha kwa jina la kutia njonjo kwenye Sanaa yake kwani anaelewa wasanii ni wengi na vitu vidogo kama hivyo ni rahisi sana kumtoa msanii kwenye mkondo sahihi na kumtupa kwenye chochoro.
“Mimi nimechagua njia tofauti kwa sababu wasanii ni wengi na kila mtu anafanya vitu vyake. Mimi naamini njia hii niliyoichagua ni sahihi kwangu na naamini nitaweza kudumu muda mrefu na ku-maintain kwenye gemu nikiwa hivi, nikiwa salama,” Jay Melody alisema.
“Lakini pia mimi siwezi kujichanganya kwa vitu kama kubadilisha badilisha wanawake na vitu kama hivyo kwa sababu siamini sana kweney hiyo njia, ninachokiamini mimi ni kwamba hata kwenye mahusiano ni mtu kuwa permanent. Kuwa na mwanamke mmoja ambaye anaweza akakufaa ili ukaendelee na maisha yako usipatwe na stress nyingi,” aliongeza.
Mkali huyo wa ‘Nakupenda’ alisema kwamba sababu yake kuamini katika falsafa hiyo ambayo kidogo inakaa tofauti kutoka kwa falsafa za wasanii wengi wa miziki ya kizazi kipya ni kwamba huwa anavunjika oyo haraka na ili kukwepa hilo, anachagua kunata kwenye mpenzi mmoja tu sahihi.
“Mimi ni mtu ambaye vitu vidogo vidogo vinanipa sana depression yaani nakuwa na mawazo sana, kwa hiyo sitaki kujichanganya kwa wadada hawa watanipoteza. Wadada wa mjini tuwaachie tu wasanii ambao wanaona kabisa wana uwezo wa kupambana nao. Mimi ni mtu ambaye mara nyingi hata nazima simu ili niwe na Amani tu,” alisema.
Jay Melody alisema kwamba licha ya kuwa mtu anayependa mitoko sana lakini hatumii kilevi chochote.