logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Raila akosa pa kuficha uso MCA wa kike wa Turkana akimkabili kwa maswali magumu hadharani

Kuya alidai kwamba eneo hilo linampenda Odinga kama Yesu lakini yeye amewalipa kwa chuki kama shetani.

image
na Radio Jambo

Habari14 October 2023 - 07:21

Muhtasari


• Kuya alidai upendo wa eneo hilo kwa mwanasiasa huyo mkongwe unalinganishwa tu na ule wa Yesu wa kibiblia, akidai kuwa Raila amewalipa tu kwa dharau.

MCA wa Turkana amkabili Raila Odinga maswali.

Ijumaa wakati wa hafla ya kusherehekea utamaduni na utalii wa kaunti ya Turkana unaojumuisha jamii kutoka mataifa matatu ambao wanazungumza lugha moja, mwakilishi wa wadi ya Lodwar Township Ruth Kuya alimkabili kiongozi wa upinzani Raila Odinga na maswali magumu.

Odinga alikuwa mmoja wa viongozi wakuu waliohudhuria hafla hiyo ya kitamaduni na kwa ishara zote hakuwa amejipanga kukabiliwa na maswali ya kijasiri kutoka kwa mwanasiasa huyo mchanga wa kike.

Kuya, kwa ujasiri alimzomea Odinga hadharani huku akimuuliza maswali magumu kwa kile alidai kwamba kiongozi huyo wa ODM amekuwa akitenga jamii za kutoka eneo hilo licha ya kuwa wengi wao wamekuwa wakimuunga mkono katika chaguzi za awali.

Kuya alidai upendo wa eneo hilo kwa mwanasiasa huyo mkongwe unalinganishwa tu na ule wa Yesu wa kibiblia, akidai kuwa Raila amewalipa tu kwa dharau.

"Siogopi kuongea. Gavana na wageni waheshimiwa. Ninachotaka kusema ni kwamba Raila anastahili kukaribishwa kama babu eneo hili; ni utamaduni wa watu wa Turkana. Raila, unaheshimiwa. Sisi Waturkana watu wanakupenda kama Yesu, na ulionekana kutuchukia kama shetani. Badala ya kutupatia uteuzi, unampa binti yako. Vijana wako taabani, na wanahitaji kazi," Kuya alimzomea.

Alihoji ni kwa nini Raila bado hajaajiri kijana yeyote kutoka eneo hilo kufanya kazi katika afisi yake licha ya kuwa mwaminifu kwake.

"Umetuma wangapi ofisini kwako babu yetu tunakupenda, hatukuchukii bali tunalia kama watoto wako. Naomba kuuliza ofisi yako kwanini usituajiri? Turkana tumewahi kupokea uteuzi?" aliuliza.

Baadae, vurugu zilizuka katika hafla hiyo baina ya wafuasi wa Odinga na wale wa gavana Jeremiah Lomorukai na baadae Mbunge wa Turkana ya Kati Joseph Namuar alichukua kipaza sauti na kutangaza kwamba wageni kutoka Nairobi wanapaswa kuondoka kwa kurejelea Raila na wenzake wake. Raila aliondoka.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved