Takriban watu watano walilazwa hospitalini wakiwa na majeraha baada ya kupigwa risasi wakati wa makabiliano kati ya polisi na mshukiwa anayesakwa.
Waathiriwa waliolazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta walipata majeraha mbali mbali baada ya nyumba zao kumiminiwa risasi wakati mshukiwa wa wizi aliyekuwa akisakwa alipigwa risasi na kuuawa katika majibizano ya risasi katika eneo la Githurai, Nairobi.
Polisi walisema Samuel Karui almaarufu Sammy Steppa alisakwa kwa msururu wa wizi, vurugu na matukio ya mauaji katika eneo la Kasarani na viungani mwake.
Alikabiliwa na polisi katika nyumba ambayo ilisemekana kuwa ya mpenzi wake wakati alipokuwa amemtembelea.
Polisi walisema kuwa mwenzake alifanikiwa kutoroka ingawa walipata bastola. Kamanda wa polisi Nairobi Adamson Bungei alisema wanachunguza tukio hilo.
“Tutafuatilia suala hilo,Waliojeruhiwa hali zao zinaendelea vizuri hospitalini," alisema.
Mpenzi wa mshukiwa huyo alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa uchunguzi zaidi.
Mwezi uliyopita, afisa wa polisi alipigwa risasi na kuuawa huku wengine watatu wakijeruhiwa katika makabiliano sawa na hayo katika eneo hilo hilo.