Mchekeshaji na Mwigizaji Jacky Vike maarufu Awinja amefunguka na kusimulia sababu ya makalio yake kuwa madogo kinyume na akina dada wenzake kutoka Magharibi.
Wakati wa mahojiano na Oga Obinna, Awinja alitania kwamba makalio yake madogo,yalisababishwa na jinsi alivyokuwa akisafiri hadi nyumbani kwao kijijini alipokuwa mdogo.
“Nimezaliwa Nairobi. Lakini sisi tulikuwa tunaenda kijijini sana. Kama kila sikukuu na wakati tukifunga shule ikiwepo Aprili, Agosti, Desemba, sheria za baba yangu lazima tungeingia Kabiet Escort. hizi ni zile basi za kitambo kabla Ugwe, Homeboys, Eldoret Express, ile engine yake ilikuwa ndani ya basi so tulikuwa tunakalia hio engine ndio maana mimi niko na makalio madogo. Ilichomeka mtu wangu, iliiva ulikuwa unafika nyumbani haga inawaka moto,"alisema.
Kama kusisitiza , Awinja alisema kwamba siku hizo, safari zilikuwa ndefu sana.
"Siku hizo safari zilikuwa ndefu sana, fupi zaidi ilikuwa kama masaa 8. Unapoondoka saa 5 asubuhi, utafika saa 4 au 3 usiku. Mambo yamebadilika siku hizi tunasafiri kwa saa sita,” alibainisha.
Wakati huo huo alifichua ni lini mara ya mwisho alitumia usafiri wa umma hadi nyumbani kwake kijijini,akifafanua utofauti wa jinsi ya kusafiri kwenda kijijini na jinsi ya kusafiri kwenda ngambo.
“Utamu wa kwenda mashambani sidhani kama ni kwa ndege. Siwezi kwenda Ulaya kwa ndege na kisha kwenda kijijini kwenye ndege tena. Lazima kuwe na tofauti. Inabidi uende kwa basiili ufurahie mazingira. Mara ya mwisho kupanda basi ilikuwa mwaka huu. Haikuwa kuigiza, ilikuwa ni kujifurahisha tu nikitoka nyumbani, nilikuwa na Shix(Kapienga) tulikaa nyuma. Tulirushwa tulirushwarushwa mpaka tukafika,” alisema.