Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Ann Waiguru amewapongeza Maseneta kwa kuchagua kumpa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza nafasi nyingine ya kutawala kaunti hiyo.
Katika taarifa yake Alhamisi, Waiguru ambaye pia ni Gavana wa Kirinyaga aliwapongeza maseneta hao kwa kupiga kura wakiwa na dhamira ya kumpedekeza Kawira arudi madarakani.
"Kwa maseneta wanaowakilisha kaunti 47, asanteni kwa kupiga kura kwa dhamiri zenu," alisema.
Akisherehekea ushindi wa Mwangaza, Waiguru alimpongeza kwa kuonyesha uso wa kijasiri wakati wote wa kesi yake.
"Hakika - Asiye na wake ana Mungu, wakati wa changamoto na mabishano ndio nguzo ya kweli ya uongozi," alisema.
Akitoa ushauri wake Gavana wa kaunti ya Kirinyaga alimtaka Mwangaza kuwaongoza wakazi wa Meru kwa utoaji huduma.
"Kwa dada yangu Gavana Kawira Mwangaza, ni kwa sasa ujasiri wa kuendelea mbele na kwa umakini kutumikia kaunti yako ndio muhimu," Waiguru alisema.
Bunge la Seneti lilitupilia mbali mashtaka yote katika kura, na hivyo kumpa Mwangaza maisha mapya katika uongozi wa kaunti.
Alikabiliwa na mashtaka ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya rasilimali, upendeleo, uonevu, uteuzi usio halali, kudharau mahakama, na kuipa barabara jina la mumewe kinyume cha sheria.