Wanafunzi wanne wa kidato cha nne walikamatwa kwa madai ya kuvuta bangi shuleni mjini Kisumu.
Wanafunzi hao wanne walikamatwa Jumatatu jioni na baadaye kuachiliwa na polisi ili kuruhusiwa kufanya mtihani wa KCSE unaoendelea kabla ya kushtakiwa mahakamani ripoti ya polisi ilisoma.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo alisema kuwa wanafunzi hao walionaswa walikuwa wametumia funguo za shule kufikia ofisi ya michezo ambapo walipatikana wakivuta bangi.
Wakati wa kukamatwa, misokoto saba ya bangi ilipatikana na kuwekwa kama ushahidi. Wanne hao ni wa umri wa kati ya miaka 17 -18.
Kulingana na shirika la NACADA pombe, tumbako, bangi, miraa na dawa za kulevya ndizo zinazotumiwa vibaya zaidi shuleni.
Utafiti wa kitaifa wa miaka mitano kuhusu Hali ya Dawa na Matumizi ya Dawa za Kulevya nchini Kenya, 2022 uliotolewa hivi karibuni unaonyesha watoto 156,461 wa shule za msingi kwa sasa wanatumia tumbaku.
127,124 wanatumia pombe, Miraa 112,456 na 39,115 wanavuta bangi.
Mtafiti Mkuu wa Nacada Morris Kamenderi alisema kwa jumla, vijana 153,846 wenye umri wa miaka 15 hadi 24 tayari wameathirika sana na pombe.
Huku vijana 90,531 wakitajwa kuathirika na uvutaji wa bangi.
Wiki iliyopita, shirika la afya duniani lilipendekeza kupiga marufuku uuzaji wa bidhaa hizo karibu na shule.
Sheria ya Kudhibiti Tumbaku nchini Kenya tayari imepiga marufuku uuzaji wa bidhaa za tumbaku karibu na shule.