logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Raila asema ufisadi umechangia kupanda kwa bei ya petroli

Alisema mkataba kati ya Kenya na Saudi Arabia ni wa kunufaisha watu wachache.

image
na Radio Jambo

Habari16 November 2023 - 13:43

Muhtasari


• Raila pia alikosoa serikali kwa kuwaficha wakenya maelezo kuhusu mkataba huo, akiutaja kuwa ni "ulaghai" ambao lengo kuu lilikuwa kuwadhulumu Wakenya kama watumiaji wa mwisho wa mafuta.

Kinara wa Azimio Raila Odinga anataka tume ya kukabiliana na ufisadi nchini EACC kuanzisha uchunguzi wa haraka ili kuwachukulia hatua wahusika wa sakata ya mafuta ambayo imechangia kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli nchini Kenya licha ya bei kushuka kimataifa.  

Akihutubia mkao wa wanahabari siku ya Alhamisi Raila pia alitaka makampuni yanohusika kuchunguzwa na kutahmini ikiwa yamekuwa yakilipa ushuru kama inavyotakikana kisheria.  

Kingozi huyo alielezea hofu kuwa huenda gharama ya mafuta nchini ikapelekea nchi kama vile Uganda kubadili mkondo na kuanza kuagiza mafuta yao kupitia nchi ya Tanzania. Raila alidai kuwa baadhi ya viongozi katika serikali wamekuwa wakiwafilisi wakenya mabilioni ya pesa kwa kuongeza bei ya mafuta ya petroli na dizeli.

Alisema kuwa mkataba uliyotiwa saini kati ya serikali ya Kenya na Saudi Arabia ulinuia kufyonza wakenya na kunufaisha watu wachache wenye ushawishi serikalini.  Raila alidai kuwa bei ya sasa ya mafuta imepandishwa kwa shilingi 30 kutokana na mkataba wa ulaghai uliyotiwa saini na serikali.

Kiongozi huyo wa Azimio anadai kuwa baadhi ya wandani wa serikali ndio wanaonufaika na ongezeko la shilingi 30 kwa kila lita ya mafuta ya petroli na dizeli.  

“Bei halisi ya mafuta ya petroli ingekuwa shilingi 187 kwa lita lakini sasa watu wafisadi kwenye serikali wamesikizana kuongeza  bei hadi shilingi 217,” Raila alisema. 

Aliongeza kuwa, “...hakukuwa na G-to-G. Kenya haikutia saini mkataba wowote na Saudi Arabia au UAE. Wizara ya Kawi na Petroli pekee ndiyo iliyosaini mkataba na makampuni ya serikali ya mafuta katika Mashariki ya Kati.” 

Raila pia alikosoa serikali kwa kuwaficha wakenya maelezo kuhusu mkataba huo, akiutaja kuwa ni "ulaghai" ambao lengo kuu lilikuwa kuwadhulumu Wakenya kama watumiaji wa mwisho wa mafuta. 

"Utagundua kuwa meli zinachukua muda mrefu kabla ya waagizaji kuthibitishwa, na malipo yanaendelea kuongezeka. Bei ya kushikilia meli kwa siku imeongezeka kutoka dola 45,000 hadi dola 70,000, na yote haya yanapitishwa kwa mtumiaji,” Raila alisema.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved