Takriban watu 37 wamefariki katika mkanyagano kabla ya zoezi la kuwasajili makurutu wa kujiunga na jeshi katika uwanja wa michezo nchini Congo-Brazzaville, maafisa wamesema.
Baadhi ya watu walijaribu kupita kwa nguvu katika lango la uwanja wa michezo katika mji mkuu, Brazzaville, na kusababisha mkanyagano huo, wakaazi wamenukuliwa wakisema.
Wiki iliyopita, jeshi lilitangaza mipango ya kuajiri takriban watu 1,500 kati ya umri wa miaka 18 na 25.
Haijabainika ni watu wangapi walijeruhiwa katika ajali hiyo ya usiku kucha.
Taarifa ya serikali ilisema kuwa "kitengo cha kupambana na mgogoro" huo kimeanzishwa, shirika la habari la AFP linaripoti.
Kulingana na shirika la Associated Press, watu wengi kama 700 kwa siku wamekuwa wakijiandikisha katika wiki iliyopita katika vituo vya kuajiri.
Jumatatu usiku, maelfu ya vijana waliripotiwa kujitokeza katika uwanja wa Michel d'Ornano kuwa wa kwanza kwenye mstari Jumanne.