Wakazi wa Kijiji cha Busagula katika Halmashauri ya Mji wa Kigangazi, Wilaya ya Bukomansimbi nchini Uganda walishuhudia kisanga cha taharuki baada ya mti ulioanguka miaka saba iliyopita kuinuka.
Kwa mujibu wa Nile Post, Wakaazi kutoka vijiji tofauti walikusanyika kushuhudia mti huu ulioinuka bila msaada wa mtu yeyote.
Wenyeji walisimulia kuwa mti huo, ulikua kwa miaka 30 baada ya kupandwa lakini mnamo 2016 mvua kubwa iliuangusha.
Walakini, wiki hii walishangaa baada ya mti kuinuka.
“Wote ilianguka chini hata mizizi ilikuwa nje ya ardhi. ”
Mti upo katika bustani ya mkulima mmoja kwa jina Enock Mukalazi, mkazi wa Busagula, katika Halmashauri ya Mji wa Kigangazi Wilaya ya Bukomansimbi.
Wakazi waliambia jarida hilo kuwa mti huo uliwashangaza kulingana na mwonekano wake.
"Wiki iliyopita nilichota kuni kutoka kwa mti huu wa Mutuba na nimekuwa nikiokota kuni kutoka kwake lakini nilishangaa nilipoambiwa kuwa uliinuka," Tusasirwa Florence mkazi wa kijiji cha Busagula alisema.
Baadhi ya wakazi hao wameona hii ni baraka kutoka kwa Mungu na wengine wameanza kuweka sarafu na mbegu za kahawa chini ya mti huku wakipiga magoti kuomba baraka kutoka kwa mababu zao.
Wakazi hao walisema kuwa hii si mara ya kwanza kuona maajabu hayo kijijini kwao bali wanauliza kwa nini huwa ni wao kila mara.