KAMPUNI ya kusambaza umeme nchini Kenya (KPLC) imeonya kuhusu kukatizwa kwa umeme katika maeneo kadhaa nchini siku ya Jumatatu.
Katika taarifa ya Jumapili jioni, kampuni hiyo ilitangaza kwamba maeneo kadhaa katika kaunti tano za Kenya yatakosa umeme kati ya saa mbili asubuhi na saa kumi na moja jioni. Kaunti ambazo zitaathirika ni pamoja na Kiambu, Kajiado, Turkana, West Pokot, na Embu.
Katika kaunti ya Kiambu, sehemu za maeneo ya Kwa Maiko na Mitahato zitaathirika na kukatizwa kwa umeme kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi na moja jioni. Miongoni mwa sehemu zitakazoathirika ni pamoja na Raini, Ruiru Mills, Oakland, Kambui Girls, Jacaranda Waters na viunga vyake.
Sehemu za maeneo ya Kajiado, Kisaju na Isinya katika kaunti ya Kajiado pia zitakuwa bila umeme kati ya saa mbili asubuhi na saa kumi na moja jioni.
Baadhi ya sehemu za eneo la Kalemngorok katika kaunti ya Turkana zitaathirika na kukatizwa kwa umeme kati ya mbili asubuhi na saa kumi na moja jioni.
Katika kaunti ya West Pokot, sehemu za eneo la Cemtech zitaathirika na kukatizwa kwa umeme kati ya saa mbili asubuhi na saa kumi na moja jioni.
Sehemu za maeneo ya Mayoiri Mariari na Kiambere katika kaunti ya Embu zitakosa umeme kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi alasiri.