Mtumbuizaji mashuhuri nchini Kenya Allan Ochieng almaarufu Hype Ballo ameachiliwa kwa dhamana ya KSh500,000 katika kesi ya mauaji ya afisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) katika Kaunti ya Kiambu.
Hype Ballo, ambaye ni mshukiwa mkuu wa mauaji ya afisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Felix Kintosi, ameachiliwa kwa bondi ya Ksh.500,000 na mdhamini wa kiasi sawa na hicho au njia mbadala ya dhamana ya pesa taslimu Ksh.500,000.
Hype Ballo aliachiliwa Jumatano na Jaji wa Mahakama ya Kiambu Dorah Chepkwony kwa sharti kwamba ahudhurie vikao vyote vya mahakama.
Pia aliagizwa kuripoti katika afisi ya DCI ya kaunti ndogo ya Kikuyu siku ya kwanza ya kila mwezi hadi shahidi mkuu atakapotoa ushahidi wake, na pia anatarajiwa kusalia chini ya uangalizi wa chifu wa eneo la Kibera hadi kesi yake itakapokamilika.
Kesi itatajwa Mei 22, 2024, kwa ajili ya kupanga tarehe ya kusikilizwa.