Idara ya Sheria ya Marekani inasema inazingatia iwapo itawafungulia mashtaka Boeing kutokana na ajali mbili mbaya zilizohusisha ndege yake ya 737 Max.
Kampuni hiyo kubwa ya usafiri wa anga ilikiuka masharti ya makubaliano yaliyofanywa mwaka wa 2021 ambayo yalilinda kampuni hiyo dhidi ya mashtaka ya uhalifu yanayohusishwa na matukio hayo, Idara hiyo ilisema.
Boeing imekanusha kuwa ilikiuka makubaliano hayo.
Ajali hizo - moja nchini Indonesia mnamo 2018, na nyingine nchini Ethiopia mnamo 2019 - ziliua jumla ya watu 346.
Mtengenezaji wa ndege alishindwa "kubuni na kutekeleza mpango wa kufuata maadili ili kuzuia na kugundua ukiukaji wa sheria za ulaghai za Marekani katika shughuli zake zote," Idara ya sheria ya Marekani ilisema.
Boeing ilisema inatazamia fursa ya kujibu Idara hiyo ya Sheria na kwamba "inaamini kuwa ili heshimu masharti ya makubaliano hayo".
Chini ya mpango huo, Boeing ililipa malipo ya $2.5bn (£1.98bn), huku waendesha mashtaka wakikubali kuiomba mahakama kufuta shtaka la uhalifu baada ya muda wa miaka mitatu.
Idara ya Sheria ilisema Boeing ina hadi Juni 13 kujibu madai hayo na kwamba kile ilichosema kitazingatiwa inapoamua nini cha kufanya baadaye.
Jamaa wa waathiriwa wametaka kampuni hiyo kuchukuliwa hatua za uhalifu.
"Hii ni hatua nzuri ya kwanza, na kwa familia, muda mrefu unakuja. Lakini tunahitaji kuona hatua zaidi kutoka kwa Idara ya sheria kuwajibisha Boeing," mwanasheria wa familia za wahasiriwa Paul G Cassell alisema katika taarifa.
Boeing imeendelea kukabiliwa na uchunguzi mkali kuhusu usalama wa ndege yake baada ya mlango ambao haujatumika kufunguka kwenye ndege aina ya 737 Max muda mfupi baada ya kupaa mwezi Januari, na kuacha pengo ubavuni mwa ndege hiyo.